Takriban watu 700 wanaoishi kando ya Mto Tana—eneo lenye hatari ya mafuriko katika kaunti za Garissa na Tana River—wanatarajiwa kuhama na kwenda maeneo ya juu kabla ya kuanza kwa mvua za miezi ya Oktoba, Novemba na Disemba, huku juhudi za kujiandaa kukabiliana na majanga zikiongezwa kasi. Wakaazi wa vijiji vya Mororo, Bakuyu, Ziwani, Deri na Mathengeni walihimizwa kuzingatia tahadhari za mapema wakati wa mafunzo ya kujiandaa kukabiliana na majanga yaliyoendeshwa Jumamosi na shirika la Helping Hand for Relief and Development. Mkuu wa programu za shirika hilo, Yussuf Ibrahim, alisema kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu sana katika kulinda maisha na mali.