Watu wanne wamefariki na wengine 16 kujeruhiwa kufuatia ajali ya barabarani katika eneo la Riverland, kwenye barabara ya Meru kuelekea Nkubu, usiku wa kuamkia leo. Ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa lori kudaiwa kupoteza mwelekeo na kutoka nje ya barabara, kisha kugonga magari kadhaa na wafanyabiashara waliokuwa kando ya barabara. OCPD wa North Imenti Hassan Bashir, alithibitisha tukio hilo na kusema kuwa timu za uokoaji zilifika eneo la tukio. Majeruhi walikimbizwa hospitalini, huku miili ya waliofariki ikipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Meru.