Mamlaka ya KRA imenasa tani 46 za sukari inayoshukiwa kuingizwa nchini kwa njia ya magendo huko Lodwar, Kaunti ya Turkana, katika operesheni inayolenga kukomesha biashara haramu ya kuvuka mpaka. Operesheni hiyo, iliyoongozwa na taarifa za kijasusi na kufanywa mapema jana, ilipelekea kunaswa kwa malori mawili yaliyokuwa yamebeba jumla ya magunia 920 ya sukari. KRA imesema kuwa shehena hiyo ilikuwa na thamani ya ushuru wa Shilingi milioni 9.73, huku ikionya kuwa biashara ya magendo inadhoofisha ukusanyaji wa mapato na biashara ya haki.