IEBC imemwamuru Mbunge wa Nakuru Town East, David Gikaria, kulipa faini ya Shilingi milioni 2.5 na kuomba radhi kwa umma baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi lake la kupinga adhabu zilizowekwa dhidi yake kutokana na vitendo vya kuhonga wapiga kura na kueneza taarifa potofu wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou. IEBC ilieleza kuwa Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, ilitupilia mbali ombi la Gikaria la kutaka mahakama ipitie upya uamuzi huo, hatua inayofungua njia ya kutekelezwa kwa uamuzi wa Kamati ya Kusimamia Kanuni za Maadili ya Uchaguzi uliotolewa tarehe 14 Julai mwaka huu.