Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Tharaka-Nithi, Susan Ngugi, ametilia shaka takwimu zinazoonyesha kuwa asilimia 27 ya wanawake na wasichana katika eneo la Igambang’ombe wamewahi kufanyiwa ukeketaji. Ngugi anataka kupatikana kwa takwimu sahihi na zinazoweza kuthibitishwa kuhusu suala hilo, akisema hajawahi kusikia kuhusu kukamatwa kwa watu na polisi au machifu kuhusiana na ukeketaji, wala kuokolewa kwa watoto baada ya kufanyiwa kitendo hicho. Aliyasema hayo wakati wa kongamano la uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii lililoandaliwa na Bodi ya Kupambana na Ukeketaji huko Kathwana.