Mahakama ya Mombasa imempata na hatia mfanyakazi wa benki, Hannington Muthoka, kwa kosa la jaribio la mauaji baada ya kumdunga kisu mara tatu mpenzi wake wa zamani, Elizabeth Shigari, na kuacha sehemu ya kisu mgongoni mwake. Hakimu Mkaazi Mwandamizi David Odhiambo alimpata na hatia Muthoka kwa jaribio la kusababisha kifo cha Shigari kinyume cha sheria mnamo Septemba 2023, eneo la Port Reitz, Changamwe. Mahakama iliamua kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi yake pasipo shaka yoyote baada ya kuita mashahidi kumi.