Waziri wa Afya Aden Duale ametetea mageuzi ya ufadhili wa sekta ya afya nchini Kenya, akisema kuwa SHA ni muhimu katika kupanua upatikanaji wa huduma bora za afya huku ikipunguza mzigo wa kifedha kwa jamii. Duale anasema kuwa hazina tatu za SHA — hazina ya Huduma za Afya ya Msingi, hazina ya Bima ya Afya ya Jamii, na hazina ya Huduma za Dharura, Magonjwa Sugu na Mahututi — ni sehemu ya juhudi za kujenga mfumo wa afya ulioratibiwa vyema na endelevu, pamoja na kuharakisha utekelezaji wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC).