Mahakama ya Nairobi leo inatarajiwa kuamua kuhusu kama Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai inaweza kuendelea kuwazuilia Rose Mbithe na mwanawe, Chris Mulwa, kwa siku 30 zaidi kuhusu mauaji ya mwanasaikolojia maarufu Dkt. Victoria Mutiso. Wawili hao ni miongoni mwa washukiwa wanaohusishwa na shambulio la risasi lililosababisha kifo katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi Jumatano iliyopita. Uchunguzi wa maiti uliofanywa wiki iliyopita ulibaini kuwa Dkt. Mutiso alifariki kutokana na kutokwa na damu nyingi baada ya kupata majeraha matatu ya risasi.
Wakati huo huo, washukiwa wengine wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo. Angela Mulwa na Nelson Masiga wanatarajiwa kufikishwa mahakamani asubuhi ya leo.