NAIROBI, KENYA, Agosti 4, 2025 — Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, ameituhumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kununua tiketi zote za mechi kati ya Harambee Stars na DR Congo, akidai ilikuwa njama ya kuzuia maandamano ya wapinzani katika Uwanja wa Moi, Kasarani.
Seneta Sifuna alidai kuwa serikali ilihofia uwepo wa wafuasi wa upinzani waliokuwa wamepanga kutumia mechi ya Jumapili kama jukwaa la kutoa ujumbe wa kupinga serikali kwa kuimba maneno ya “Wantam” (ikimaanisha 'Wanga') wakati wa mechi ya kuwania kufuzu kwa CHAN 2024.
“Wakora wa hii serikali wamenunua tikiti zote ati ndio watu wa Nairobi wasiende uko kuimba ‘Wantam’. Pahali popote tuko tutaimba,” alisema Sifuna akihutubia wanahabari baada ya mechi.
Kiongozi huyo wa chama cha ODM pia aliongeza kuwa kupokonywa kwa mashabiki nafasi ya kuhudhuria mechi ni kielelezo cha serikali kuogopa sauti ya wananchi.

Kalonzo Naye Alitilia Shaka Mfumo wa Uuzaji wa Tiketi
Kauli ya Sifuna inakuja saa chache baada ya Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, kusema kuwa mchakato wa kuuza tiketi ulijawa na hila na ukosefu wa uwazi.
Kalonzo alikuwa amesema kuwa "watu wachache walipewa idhini ya kununua tiketi nyingi," jambo alilodai limewanyima mashabiki wa kawaida nafasi ya kushuhudia mchezo wa kihistoria.
LOC Yakana Madai Yote: "CAF Ndiyo Waliuza Tiketi"
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano (LOC), Nicholas Musonye, alikanusha madai hayo katika mahojiano na runinga ya NTV usiku wa Jumapili.
"Hakukuwa na ununuzi wa tiketi kwa njia ya uficho. Tiketi za Harambee Stars dhidi ya DRC zilikuwa wazi sokoni. Fikra kwamba tulipeana tiketi kwa watu fulani si ya kweli. Tiketi hizi ziliuzwa na CAF kupitia majukwaa yao wenyewe," alisema Musonye.
Musonye alisisitiza kuwa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ndilo lililochagua majukwaa ya uuzaji, na LOC haikuhusika na mchakato huo moja kwa moja.

Hali ya Sintofahamu Yatanda
Mashabiki wengi walielezea kupitia mitandao ya kijamii kuwa walikosa tiketi licha ya kujaribu kuzifikia mapema, huku baadhi wakidai kwamba tovuti rasmi ya uuzaji ilionyesha kuwa tiketi zimekwisha hata kabla ya mechi kuanza.
Kiongozi mmoja wa vijana kutoka Kibra alisema, “Tulikuwa tumepanga kwenda kushangilia timu ya taifa, lakini tiketi hatukuziona. Sasa tunasikia eti walinunua zote kimakusudi?”
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!