Martha Karua

KIONGOZI wa chama cha People’s Liberation Party, PLP Martha Karua amedokeza kwamba ni wakati sasa Kenya kuongozwa na rais mwanamke.

Akizungumza Jumatatu katika kaunti ya Isiolo, Karua aliweka wazi nia yake ya kuwania urais, akisema kwamba atalitunza taifa la Kenya kwa njia sahihi ya upendo kama jinsi ambavyo mama hutunza boma lake.

“Kile kiti mimi nataka ni cha urais. Na ndivyo kama mama niweze kutunza Kenya vile ambavyo mama hutunza boma. Mama hawezi kuacha mtoto hata mmoja kulala njaa. Hata chakula kikiwa kidogo mama anagawa kidog-kidogo ili kila mmoja apate, hata mtu wa kupita anapatiwa yake kidogo,” Martha Karua alisema.

Kiongozi huyo ambaye tangu kusambaratika kwa uliokuwa muungano wa upinzani wa Azimio amekuwa akiikosoa serikali mara kwa mara amekuwa akionekana kuweka hai matumaini yake ya kuliongoza taifa.

Alisema kwamba Kenya ina utajiri wa kipekee ambao unafaa kumfaidi kila mwananchi, akionekana kuashiria kwamba ilivyo kwa sasa, kuna upendeleo katika ugavi wa raslimali za taifa.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Keki ya Kenya tunataka igawe kwa usawa, sio vile ilivyo siku hizi. Mmejaribu wanaume huo wakati wote lakini safari hii nawaomba mjaribu mama kupitia PLP,” Karua alirai wananchi.

Karua ameonekana kukubali Ushirikiano na viongozi wengine wa upinzani akiwemo aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka katika kuzindua muungano dhabiti wa kushindana na rais Ruto katika uchaguzi wa urais 2027.

Cha ajabu ni kwamba licha ya viongozi hao wote kuonekana kuwa na nia ya kufanya kazi pamoja, kila mmoja wake kwa wakati wake amekuwa akiweka wazi kwamba atawania urais 2027.