
NAIBU wa rais, profesa Kithure Kindiki amedokeza kwamba huenda serikali ikawa na mpango wa kuwasaidia watoto wa wachungaji wa madhehebu mbalimbali kupata kazi.
Akizungumza Jumanne Aprili 15 jioni, wakati wa Kongamano la Ajenda ya Uamsho wa Afrika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, DP Kindiki alibainisha kuwa viongozi wengi wa kidini hutumia muda wao kuomba na kuwafikiria watu wengine, na kujisahau wao wenyewe na familia zao.
Alisema kwamba yeye ni kama mfano kwani babake alihudumu kama mwinjilisti na mchungaji kwa zaidi ya miaka 56 na aliona jinsi watumishi wa Mungu wanajitolea sana kutatua mambo ya waumini na kuzisahau familia zao.
“Nina ufahamu kwamba kwa sababu watumishi wengi wa Mungu wanatumia muda mwingi wakiomba na kuwafikiria watu wengine, mara nyingi huwa hawana muda wa kuombea familia zao na wao wenyewe.”
“Ninasema hili kutoka eneo la uzoefu, tayari nimeshawaambia kwamba nilikulia katika boma la mchungaji. Tungependa kujitolea kwenu tena kupitia kwa huduma hii tutakuwa na uwezo wa kusapoti baadhi yenu ambao mna watoto na watu ambao mgependa sisi tusapoti kupata fursa za kazi kuhudumiwa taifa lao katika ngazi mbalimbali,” Kindiki alieleza.
Kindiki pia alisema serikali itajitolea kusaidia makanisa kupata hatimiliki za mali wanayomiliki ili kumaliza mizozo ambayo mara nyingi huwa inakumba mali yanayomilikiwa na mashirika ya kidini.
Wakati huo huo, DP aliwataka viongozi wa dini kutoa ukosoaji wenye kujenga kwa serikali kwa upendo.
Kindiki alibainisha kuwa utawala wa Kenya Kwanza ni serikali inayosikiliza na itarekebisha inaporekebishwa na makasisi.
“Biblia inasema hakuna mamlaka isipokuwa ile inayotoka kwa Mungu, kusema hivyo haimaanishi kwamba usitusahihishe tunapokosea, tunachoomba ni kuturekebisha kwa upendo.”
"Msizungumze nasi kana kwamba zaidi ya marekebisho mna masuala mengine. Jukumu lenu ni kuturekebisha na kuturudisha nyuma na sisi ni serikali inayosikiliza, tutasikiliza na kurekebisha pale ambapo hatufanyi vizuri," Kindiki aliongeza.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!