
MBUNGE wa Kapseret Oscar Sudi kwa mara ya kwanza amezungumzia Kauli zinazozunguka kitembo chake cha kielimu.
Akizungumza Jumapili katika Eneobunge la Kiambaa, Sudi alikiri waziwazi kwamba wanaosema hajasoma wanasema ukweli, huku akijitetea kwamba hakuna mahali amewahi simama na kupingana na Kauli hiyo.
Hata hivyo, Sudi alijipiga kifua kwamba licha ya kuambiwa hajasoma, katika Eneobunge lake amepanga masuala ya maendeleo hata kuwashinda wale wanaojidai kuwa wasomi.
“Mimi niwaulize nyinyi, si mnasikia wanasema mimi sikuenda shule? Mnafikiri hao watu wanasema uongo? Mmewahi sikia mahali nikisema nilienda shule? Lakini ukikuja huko kwangu nimepanga maneno rafiki yangu kwa sababu ya ukarabati,” Sudi alisema.
Sudi alisema kwamba watu wachache tu ndio wamesema humu nchini huku akidai kwamba sasa hivi hata akisimama urais anaangusha wengi wanaojidai kuwa wasomi.
“Hata nikisimama urais si naangusha hawa? Sisi watu wa hoe hae ndio wengi,” Oscar Sudi aliongeza.
Mwezi Februari, Sudi alipapurana kwenye mitandao wa X na seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna wakati seneta huyo alipomkashifu Ruto kwa kujihusisha na watu wasio na elimu akimtolea mfano mbunge huyo ambaye ni mwandani wa rais.
“Ruto alituambia kwamba ana PhD, mimi sijawahi ona mtu wa PhD anayetembea na mtu aliyeachia shule darasa la pili. Inawezekana aje wewe una PhD na unatembea na Sudi. Inawezekana aje hiyo kuwa ukweli,” Sifuna alisema katika mahojiano na runinga ya Citizen TV.
Hata hivyo, Sudi alimfokea Sifuna akimwambia kwamba yeye hana hata robo ya ujuzi wake, kando na kitembo cha masomo.
“Sifuna unaweza jilinganisha na mimi? Unajua IQ yangu na yako hazilingani hata kwa robo. Tafuta mtu mwingine ambaye unaweza jilinganisha naye au mwenye utalinganisha na Ruto,” Sudi alimwambia.
“Mimi niko katika kiwango changu na sio kwamba ninaringa au nini lakini unaweza ulizia kuhusu historia yangu. Huna hata robo ya ujuzi wangu. Kwa hivyo usikuwe mpuuzi kuongea kama mtoto,” Sudi aliongeza.
Sudi alisema kwamba Sifuna amekuwa na hulka ya kushambulia kila mtu akidhani ni haki yake, lakini kwake amefika kwenye mwamba.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!