CHAMA cha ODM kimetoa tamko rasmi kuhusu kuhangaishwa na tafrani inayoendelea katika maigizo ya kitaifa kaunti ya Nakuru ambapo shule ya upili ya wasichana ya Butere imezua gumzo la kitaifa kufuatia igizo lao la ‘Echoes of War’.
Kupitia ukurasa wao wa X, ODM imesuta vikali serikali kwa kuingilia ubunifu wa wanafunzi katika drama za maigizo ya shuleni.
ODM ilisema kwamba serikali haifai kuingilia kati katika ubunifu wa maigizo ya wanafunzi, ikitolea mfano jinsi wanafunzi waliigiza kuhusu uongozi dhalimu wa Afrika Kusini katika filamu maarufu ya Sarafina.
“Wengi wetu ambao tulikua katika enzi ya ukombozi wa pili nchini Kenya tunaelewa kabisa igizo maarufu la Afrika Kusini la Sarafina. Ilijikita katika wanafunzi wa shule wakisimama kidete kupinga apartheid na udhalimu kwa jumla,” ODM ilisema.
“Funzo kubwa kutoka kwayo ni kwamba hata sauti za Watoto wa shule zina umuhimu, na kwa kweli kutokana na kutokuwa na hatia na usafi kwao, sauti zao ni za umuhimu mkubwa katika kuendesha mjadala wa kitaifa,” waliongeza.
Kwa kuonekana kupinga waziwazi igizo la shule ya wasichana ya Butere la Echoes of War, kupitia mahakama na hata kutuma polisi kutupa vitoza machozi katika shule walimokuwa huko Nakuru, ODM ilisema kuwa serikali ni sawa sawa imejipiga risasi mguuni.
“Taifa limefuatilia kwa mshangao tafrani inayojiri katika kongamano la kitaifa la maigizo jijini Nakuru ambapo serikali waziwazi imeingiza baridi kutokana na igizo la Butere Girls lenye mada ‘Echoes of War’”
“Katika Ushahidi wote ambao tuko nao kuhusu kukosekana kwa umakinifu kwa uongozi huu, serikali imejipiga risasi mguuni kwa kujaribu kuzima sauti za wasichana wadogo wenye sare za shule,” ODM iliongeza.
ODM ilisema kwamba kunaibuka maswali magumu wakati serikali inaonekana kuingiwa woga na Watoto wadogo wa shule ambao wanajaribu kuonyesha talanta yao katika uigizaji.
“Tungependa kulaani vikali kunyanyaswa kwa wanafunzi wa Butere Girls, wanahabari na hata watu wengine waliokwenda kuhudhuria na tunajiunga na Wakenya wengine kuitaka serikali kuwapa wanafunzi fursa ya maonyesho yao kama wengine,” ODM ilimaliza.
Taarifa ya ODM inajiri saa kadhaa baada ya mwandishi wa igizo hilo, Cleophas Malala kudaiwa kukamatwa huku polisi wakitupa vitoza machozi katika shule moja walimoweka makaazi wanafunzi wa Butere.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!