yt
KDF kushiriki katika ubomozi wa jumba Mombasa

WAZIRI wa Ulinzi, Roselinda Soipan Tuya ametuma maafisa wa jeshi, KDF katika kaunti ya Mombasa kuongeza nguvu katika shughuli za ubomozi wa jumba la ghorofa 11 lililoanza kuzama mapema mwezi huu.

Waziri Tuya alichapisha rasmi notisi hiyo katika gazeti la serikali mnamo Aprili 7 kuhusu kutumwa kwa KDF katika kuendesha shughuli hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika Aprili 9.

Jumba hilo la ghorofa 11 lililopo eneo la Kilifi Corner lilianza kuzama mnamo Aprili 2 na kuweka maisha ya wakaazi na majirani wake katika hali ya hatari.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 241 (3) (b) cha Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, Pamoja na ibara ya 31 (1) (a), (c) na 34 (2) ya jeshi la Kenya KDF, notisi inatolewa kwamba mnamo Aprili 7, 2025, KDF walitumwa kusaidia wizara ya ndani na kaunti ya Mombasa katika hali ya dharura ambapo jumba la ghorofa 11 lililopo Kilifi Corner katika Barabara ya Abdel Nasser ambalo lilianza kuzama Aprili 2 hivyo kuweka hatarini maisha ya wakazi wa majumba yaliyo karibu nalo,” notisi hiyo katika gazeti la serikali ilisomeka.

Gavana wa Mombasa, Abdullswamad Sherrif Nassir alithibitisha kuendeshwa kwa shughuli hiyo ya kuliangusha chini ghorofa hilo ambalo limetajwa kuwa tayari orofa ya chini imezama kabisa.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Operesheni ya kubomoa jengo hilo ilianza mapema Jumatano na inatarajiwa kuchukua karibu saa 8, kwani wakaazi wanaoishi karibu wametakiwa kuondoka katika nyumba zao katika eneo hilo ili kuruhusu operesheni salama.

Kulingana na Gavana wa Mombasa Abdullswamad Sheriff Nassir, wagonjwa mahututi katika hospitali ya Makadara watahamishwa kwa muda katika vituo vya afya vilivyo karibu kabla ya ubomozi kuanza.

"Watu hawafai kwenda kazini kilomita 1.2 karibu na jengo," Gavana alibainisha akitaja maeneo kama soko la Marikiti, Buxton na City Blue.

"Watu wote walio karibu watalazimika kuondoka. Hii haitaathiri nyumba yako lakini mitetemeko itaathiri masikio yako ikiwa uko karibu. Wale ambao watafanya kazi hiyo watakuwa na vifaa vya kujikinga."