
RAIS William Ruto amedokea utayarifu wake kwa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.
Akizungumza katika siku yake ya mwisho ya ziara ya Mlima Kenya katika eneo bunge la Othaya Jumamosi, kiongozi wa taifa aliradidi kwamba uchaguzi wa 2027 utakuwa kama mtihani ambao utasahihishwa na wananchi.
Kulingana naye, wananchi ndio walio na uwezo wa kuamua uchaguzi huo wa 2027 wakizingatia kazi ambayo mgombea atakuwa amefanya katika kipindi chake akiwa uongozini.
Alisema kwamba yeye hana shaka kwamba atapasi mtihani huo na kuendelea na kazi, japo pia aligusia kwamba ikitokea ameanguka basi yuko radhi kurudi nyumbani na kuendelea na shughuli zake za ukulima.
“Mtakuja kuniuliza siku ya mtihani, mimi nitakuja kufanya mtihani wangu na nyinyi ndio mtasahihisha. Nikipita mimi naendelea, nisipopita mimi naenda kulima, hakuna shida,” rais Ruto alisema.
Katika ziara hiyo, rais alitoa wito kwa kila kiongozi kufanya kazi yake na kukoma kueneza siasa, akisema kwamba kwa sasa si kipindi cha siasa bali cha kuwafanyia wananchi kazi.
“Mimi sijakuja hapa kufanya siasa, siku ya siasa iko, tumekuja hapa mambo ya maendeleo, siku ya siasa kila mmoja atavaa rangi yake tukutane uwanjani. Kwa sasa tuwachane na siasa ya kubishana, tufanyie wananchi kazi.”
“Si kila mtu afanye kazi yake jameni, pale 2027 mtakuja kusahihisha mtihani ya kila mtu, mwenye amepita aendelee mwenye ameanguka aende nyumbani. Mimi ile mlinipa naironyosha kwelikweli,” alisema huku akitania kwamba hayuko tayari kuanguka mtihani wake 2027.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!