Jack Obaka, msemaji wa MSS nchini Haiti//Screengrab-NTVKenya

JACK Ombaka, msemaji wa oparesheni ya polisi wa Kenya nchini Haiti amevunja kimya kuhusu aliko polisi wa Kenya aliyetoweka wiki mbili zilizopita nchini humo Benedict Kabiru.

Katika mahojiano ya kipekee kutoka nchini Haiti na runinga ya NTV Kenya, Ombaka alikanusha uvumi unaoendeshwa mitandaoni kwamba Kabiru alitekwa na magenge wa Haiti na kuuawa.

Kulingana na msemaji huyo wa MSS, juhudi za kumtafuta Kabiru bado zinaendelea na kwamba wamepiga hatua kubwa katika kuelekea kumkomboa kutoka mikononi mwa magenge hao akiwa hai.

“Kwanza kabisa ningependa kuripoti kwamba tumepiga hatua kubwa katika kumtafuta. Ofisa ambaye tunamzungumzia Benedict Kabiru alihusika katika oparesheni hii na wakati huo ndio alitoweka,” Ombaka alisema.

“Tunavyozungumza sasa hivi, bado tunaendelea kufuatilia aliko afisa huyo, bado amesalia kutoweka lakini nina furaha kuripoti kwamba tunatumia rasilimali zetu zote kuhakikisha tunampata na mpaka sasa tumepiga hatua muhimu,” aliongeza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kuhusu video ambayo imekuwa ikienezwa mitandaoni ikionyesha yule anayedhaniwa kuwa ni afisa huyo akiburuzwa mchangani na kuteswa na wanaodhaniwa kuwa magenge wa Haiti, msemaji wa MSS aliipuzilia mbali video hiyo akisema kwamba huenda si ya kweli.

Kwa mujibu wa Ombaka, walipofika Haiti walikuta kwamba magenge hao walikuwa wanatumia sana propaganda kuzua hofu na woga kwao, jambo ambalo wamefanikiwa kulizima kwa asilimia kubwa.

Ombaka alitilia shaka video hiyo akisema kuwa huenda ni ya AI na si ya kweli kwamba ni afisa wao – Benedict Kabiru.

“Kitu kimoja ambacho ni cha wazi hapa Haiti ni kwamba wengi wa magenge ya Haiti hujiendeleza kwa kutumia propaganda. Hiyo video inayosambazwa na haswa katika wakati huu wa ujio wa AI, kuna uwezekano mkubwa kwamba hiyo video ni ya Benedict Kabiru,” Ombaka alisisitiza.

Idara ya polisi humu nchini, NPS wiki mbili zilizopita ilitoa taarifa kuhusu kutoweka kwa afisa huyo wa polisi wakati genge la Haiti lilishambulia msafara wao uliokwama kwenye shimo linalokisiwa kuchimbwa barabarani makusudi na magenge hayo.

Tangu wakati huo, kumekuwa na uvumi mitandaoni kwamba huenda afisa huyo aliuawa na mwili wake kufichwa na magenge hao, lakini NPS na MSS wamesimama imara kukanusha wakisema kwamba juhudi za kumtafuta zingalipo na atapatikana akiwa hai.