
WATU wasiojulikana walitatiza kwa muda ibada ya kanisa iliyohudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Aprili 6, 2025.
Kundi la vijana lilijaribu kuvamia ibada katika Kanisa la PCEA Mwiki eneo bunge la Kasarani, na kuhatarisha usalama wa waumini kwa muda.
Fujo hiyo ilitokea punde tu baada ya Gachagua na msafara wake kufika kwa ibada ya Jumapili.
Katika video zilizoenezwa mitandaoni Jumapili mchana, makumi ya vijana walionekana kuingia katika kanisa hilo kwa fujo na kuwalazimu waumini kukimbilia usalama wao.
Iliwabidi walinzi wa Gachagua kufyatua risasi hewani kuwatawanya watu huku mali kadhaa zikiharibiwa yakiwemo magari.
Wakati wa mvutano huo, gari la Gachagua lilipigwa mawe, na madirisha kuvunjwa, kulingana na picha na video zilizoonekana mitandaoni.
Mpaka wakati wa kuchapishwa kwa ripoti hii, haijulikani kundi hilo la vijana walikuwa wanalenga nini wakati wa kuvamia mkutano huo wa ibada.
Uvamizi huu unajiri siku moja tu baada ya rais William Ruto kukamilisha iara yake ya wiki moja katika eneo la Mlima Kenya.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!