
MOURINE Nyaboke, mamake mtoto Sagini ambaye aling’olewa macho mwaka 2021 ameibuka na mapya akilia kufukuzwa katika kituo cha kulea Watoto katika hali ambayo aliisimulia kwa majonzi kufukuzwa ‘kama mbwa’.
Katika video ambayo ilichapishwa na Mike Sonko kwenye ukurasa wake wa X, alieleza kwamba walienda na mama mtoto huyo katika kituo cha kulea Watoto jijini Nairobi lakini mama huyo akafukuzwa.
Mama huyo ambaye alieleza tukio kama baina ya vilio, alisema kwamba baada ya kufika, alifukuzwa bila hata kupewa nafasi ya kumuoa mtoto wake.
“Kwa majina naitwa Mourine Nyaboke, mimi ndiye mamake Sagini, nimekuja kutoka Kisii juu nilipata ujumbe Sonko anataka kusaidia mtoto wangu. Nimekuja Children’s Home wakati nilifika huko walinifukuza kama mbwa, kama mwenye sijazaa huyo mtoto, nikaambiwa hata sifai kumuona,” Mama huyo alieleza huku akilia kwa uchungu.
Mama huyo alieleza zaidi kwamba wasimamizi wa kituo hicho walimzungusha wakitaka awaonyeshe barua ya kortini kutoka Kisii kabla ya kumruhusu kumuona mwanawe.
Hata hivyo, alihangaika na kupata barua zote hitajika lakini akasema kwamba licha ya kujitutua kote huko, bado alifukuzwa bila kumuona mtoto wake.
“Nimefika wanataka barua ya kortini kutoka Kisii nimepata, wanataka ya Nairobi nimepata lakini bado wamenifukuza tu hawataki kunisikiliza. Jamani si mniaidie mtoto wangu apate kutibiwa tu, hiyo tu ndio ninataka, mtoto wangu asaidike kwa sababu sina namna nyingine,” mama alilia.
Sonko alisema kwamba zaidi ya miaka 2 tangu mtoto huyo apelekwe katika kituo hicho, hajawahi fanyiwa utaratibu wowote wa kimatibabu na wamekataa mamake asimuone.
Alifichua kwamba baada ya mama mtoto kufungiwa kutomuona mwanawe, mwenyewe alipiga simu lakini pia akaanza kuzungushwa akitakikata kutoa stakabadhi kadhaa ambazo amesema amefika mwisho wa uwezo wake.
“Imagine Baby Sagini, mtoto ambaye alitobolewa macho na jamaa zake miaka 3 iliyopita, hajapata matibabu yoyote makubwa hadi leo kutokana na kukatishwa tamaa,” Sonko alifichua.
Mtoto Sagini alipelekwa katika kituo hicho akiwa kama shahidi wa kulindwa katika kesi dhidi ya jamaa zake ambao walituhumiwa kumtendea unyama huo.
Kesi hiyo ilihitimishwa miaka 2 iliyopita, na washukiwa wakuu 3, akiwemo binamu yake, shangazi yake na nyanya yake, walihukumiwa miaka 40, miaka 10 na kifungo cha miaka 5 jela mtawalia.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!