
MBUNGE wa Homa Bay Mjini, Peter Kaluma ametoa tathmini ndefu na ya kina kuhusu ziara ya rais William Ruto katika Mlima Kenya ambayo inatarajiwa kukamilika leo Jumamosi.
Kupitia ukurasa wake wa X, Kaluma amedai kwamba kinyume na matarajio ya wengi, ziara ya rais Ruto katika eneo hilo lililokuwa limefikirika kuwa lina majungu na uongozi wake imemalizika kwa mafanikio ya kipeke.
Mbunge huyo wa ODM amedai kwamba watu wa Mlima Kenya wana upendo wa dhati kwa rais Ruto, kulingana na jinsi walijitokeza kwa wingi wakiwa na furaha, akisisitiza kwamba wingi wao na furaha yao si dalili ya watu waliolipwa ili kujitokeza na kumshangilia rais.
“Gachagua na Muungano wake wa mucene walitoweka wakati Mfalme wa Mlimani alipowasili nyumbani.Watu wa Mlima Kenya wanampenda Rais Ruto. Nambari hizo na msisimko haviwezi "kukodishwa"” Kaluma alisema.
Mbunge huyo pia alimtupia vijembe aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua ambaye tangu kubanduliwa kwake amekuwa mwiba mchungu kwenye wayo wa rais Ruto, akisema kwamba amebaki na tope usoni baada ya watu kujitokeza kumkaribisha Ruto kinyume na wito wake wa kuwataka kutojitokeza.
“Uongo ambao Gachagua na washiriki wa timu yake wamekuwa wakiuza kwamba Ruto amewapa kisogo wananchi umepingwa. Kwa hakika, sote sasa tunajua kwamba Rais Ruto amepata mgao usio na uwiano wa utumishi wa umma na rasilimali za kitaifa kwa Mlima Kenya kwa gharama ya Wakenya wengine. Mlima Kenya hupata zaidi ya nusu ya bajeti ya taifa huku huduma ya umma ya Kenya ikisoma kama jambo la ukoo wa Mlima Kenya/taifa!” Kaluma alidadisi.
Kaluma alimaliza akiwataka Wakenya wote kujiunga na kukumbatia serikali jumuishi ili kuhakikisha hawaachwi nyuma kimaendeleo kwani ubia wa ODM na UDA unalenga kuingia kwa kishindo katika kila kona ya nchi kupeleka maendeleo na si siasa.
“Wacha Wakenya wote waingie Serikalini. Ni makosa kwa kiongozi yeyote kuweka jamii yoyote ya kikabila nje ya serikali ilhali Wakenya wote ni walipa kodi sawa. Kufanya hivyo kunamaanisha kulipa kodi ili wengine wale! Ndugu zangu wote wa Kamba wachukue nafasi zao serikalini - Gachagua tayari ameharibika; Kioni hana kura; Rais Uhuru ni dhaifu mno kumfanya mtu yeyote kuwa Rais; Martha hana kura! Tufinyaneni ndani sote,” alimaliza.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!