
Kundi la wapiganaji wa Palestina la Hamas linasema kuwa linaunga mkono kurejelea hatua ya usitishaji vita katika ukanda wa Gaza kupitia pendekezo lililotolewa na wapatanishi ambalo linahusisha kuachiliwa huru kwa mateka wengine watano wa Israel ili kuwe na siku 50 za kusitishwa kwa mapigano.
Khalil al-Hayya, kiongozi wa ngazi ya juu zaidi wa Hamas nje Gaza, alisema kundi hilo limeidhinisha pendekezo hilo lililotumwa na wapatanishi wa Misri na Qatar.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema pia imepokea mpango huo, na kuwasilisha "pendekezo lake mbadala kwa wapatanishi kwa ushirikiano na Marekani".
Iwapo yatakubaliwa, makubaliano hayo mapya ya kusitisha mapigano yanaweza kuendana na sikukuu ya Waislamu ya Eid al-Fitr itakayoanza Jumapili.
Marekani haijatoa kauli kuhusu suala hili.
Haya yanajiri huku vikosi vya Israel vikianzisha operesheni ya ardhini huko Rafah na kuendeleza mashambulizi ya anga katika ukanda wa Gaza, baada ya usitishaji mapigano ulioanza kutekelezwa tarehe 19 Januari kumalizika mapema mwezi huu. Pande zote mbili hazijeweza kuafikiana kuhusu awamu ya pili ya mpango huo baada ya kumalizika kwa ule wa kwanza.
Vita hivyo vilianza wakati Hamas iliposhambulia kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, na kuua takriban watu 1,200 na kuteka wengine 251 na kuwapeleka Gaza.
Israel ilijibu kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi, ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 50,000, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!