
Mvulana mwenye umri wa miaka 15 kwa sasa anapigania maisha yake katika Hospitali ya Misheni ya Litein baada ya kumla nyoka mbichi katika Kijiji cha Chemogoch, Kaunti ya Bomet.
Tukio hilo la ajabu lilizua tafrani kijijini hapo, hali iliyosababisha familia yake kumkimbiza hospitalini hapo, ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Siku ya Jumamosi jioni, Hospitali ya Misheni ya Litein ilipokea mgonjwa ambaye hakutarajiwa katika kesi isiyo ya kawaida ambayo iliwaacha wafanyikazi wa matibabu wakiwa wamepigwa na butwaa.
Kijana huyo ambaye anafanya kazi ya kuuza bia za kitamaduni alikimbizwa hospitalini baada ya kula nyoka mbichi wa kijani kibichi.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, baadhi ya wateja wake walikuwa wamemkamata na kumuua nyoka huyo, kisha kumpeleka nyumbani. Mamake alishtuka alipomgundua akiwa na nyoka huyo aliyekufa mfukoni.
"Alisema, 'Mama, ngoja nikuonyeshe,' kisha nikapiga mayowe. Alikimbia hadi kwenye kijito, akala nyoka mzima na kunywa maji," akasimulia Emmy Ruto, mamake mvulana.
Sumu ya nyoka ilipoanza kufanya kazi, wanakijiji waliingilia kati na kumkimbiza kwenye zahanati ya eneo hilo.
Hata hivyo, hali yake ilipozidi kuwa mbaya, alihamishiwa Hospitali ya Misheni ya Litein, ambako alilazwa kwenye wadi ya wagonjwa mahututi.
"Nilipojaribu kumzuia, watu waliniambia alikuwa ameumwa na nyoka huyo. Tulimfunga kamba na kumkimbiza hospitalini," John Ruto, mjombake mvulana huyo alisema.
Baada ya matibabu ya kina, madaktari waliweza kuimarisha hali yake. Baadaye alihamishwa kutoka chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kupelekwa wodi ya jumla, ambapo sasa anaendelea kupata nafuu.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!