Kiza Besigye ashtakiwa katika mahakama ya kiraia, amaliza kususia chakula

MWANASIASA mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye ameripotiwa kumaliza mgomo wake wa kula baada ya kuhamishiwa katika mahakama ya kiraia kutoka mahakama ya kijeshi alikozuiliwa kwa takribani siku 100.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Besigye amekuwa akisusia chakula kwa takribani wiki 2, ishara ya kupinga kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi sasa amerejelea chakula.

Kiongozi huyo aliwasilishwa katika mahakama ya kiraia mapema Ijumaa ambapo alifunguliwa mashtaka ya uhaini ambayo adhabu yake ni kifo katika taifa la Uganda.

Besigye, mgombea urais mara nne katika nchi hiyo ya Afrika mashariki, alikaa kwenye kiti cha magurudumu alipokuwa akikabiliwa na mashtaka katika chumba cha mahakama katika mji mkuu, Kampala.

Besigye, 68, amekuwa kizuizini tangu Novemba 16, alipotoweka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Siku kadhaa baadaye, alifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Kampala kujibu mashtaka ya kutishia usalama wa taifa.

Mahakama ya Juu ilisimamisha kesi yake ya kijeshi mwezi uliopita, ikisema jopo la mahakama ya kijeshi haliwezi kuwahukumu raia.

Familia ya Besigye, wafuasi na wengine walitaka aachiliwe mara moja, lakini aliwekwa katika gereza lenye ulinzi mkali na baadaye kuanza mgomo wa kula.

Besigye ameonekana kuwa dhaifu katika kufikishwa mahakamani hivi karibuni, na kusababisha wasiwasi kwamba madhara yoyote kwake jela yanaweza kusababisha machafuko mabaya. Raia wengi wa Uganda wanazitaka mamlaka kumwachilia huru kwa misingi ya huruma.

Besigye alirudishwa rumande hadi Machi 7, wakati anatarajiwa kurejea mahakamani.