
RAIS William Ruto amevunja kimya chake baada ya wakenya kugeuza hotuba yake ya kuzindua barabara ya kilomita 750 kaskazini mashariki mwa Kenya kuwa wimbo wa kejeli.
Wakenya wa matabaka mbalimbali kwenye mitandao wa TikTok waligeuza hotuba ya Ruto kutaja Maeneo ambayo barabara ya kilomita 750 itapitia kuwa wimbo kama njia moja ya kukejeli ahadi hiyo.
“Ndio barabara itoke Mandera, ikuje Rhamu, ikuje Garre, iende Elwak, ikuje Kobow, ikuje Kotulo, ikuje Tarbaj, ipitie pale Wajir, iende Samatar, iteremke Modogashe, ifike Isiolo,” Ruto alisema wiki tatu zilizopita wakati wa ziara ya wiki moja ya kimaendeleo katika ukanda wa Kaskazini mashariki.
Ni kauli ambayo iliwavutia Wakenya wengi haswa kwa jinsi rais alikuwa na ustadi katika kujua Maeneo mbalimbali ya eneo hilo ambalo halijakuwa na maendeleo mengi tangu Uhuru.
Wakenya pia waliikejeli kauli hiyo kupitia video fupi kwenye TikTok wakiashiria kutoamini kama rais atatimiza ahadi hiyo.
Jumatano akiwajibu, Ruto alisema kwamba ameona baadhi ya kejeli hizo akisema kwamba atatimiza ahadi ya kujenga barabara hiyo ya umbali wa kilomita 750.
“Wiki mbili zilizopita nilikuwa Kaskazini mashariki na nilitoa ahadi ya barabara ambayo itajengwa kutoka Isiolo kupitia Wajir kuelekea Mandera. Na watu wengi wanadhani au wanafikiria ni mzaha. Acha niwambieni watu wazuri, unajua katika taifa hili baadhi wanachukulia suala la kufa na kupona kwa mzaha, nimejitolea kuhakikisha barabara hiyo ya kilomita 750 kutoka Isiolo hadi Mandera kwa sababu kwa muda mrefu tumekuwa tukitelekeza Kaskazini mashariki kimaendeleo,” Ruto alijibu.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!