Mbunge wa EALA, David Ole Sankok ametaka bunge kumtengenezea nafasi ya uongozi Raila Odinga

MBUNGE wa bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki, EALA, David Ole Sankok amevutia maoni mseto baada ya kudai kwamba aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa AUC, Raila Odinga anastahili kukabidhiwa wadhifa katika bunge la kitaifa Kenya.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Ole Sankok alitoa ombi lisilo la kawaida kwa wabunge kutafuta njia ya kumbandua mamlakani mwanasiasa mmoja ili kumtengenezea Odinga nafasi ya wadhifa.

Sankok alisema kwamba wakati umefika wa Odinga kuvishwa taji akimtaja kama simba wa bara zima la Afrika.

“Bunge la Kenya linafaa kumbandua mtu ili kuunda nafasi ya Simba wa Afrika, Mfalme asiye na taji ~ Baba Raila Odinga. Tumuweke taji sasa,” Ole Sankok alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mwanasiasa huyo aliendeleza kutoa wito huo kwa wabunge akisema kwamba Odinga anaweza tengenezewa nafasi bungeni ya ama kuwa kiongozi wa wengi bungeni au spika.

“Tunaweza kuunda nafasi ya Waziri Mkuu au kutafuta fomula ya Raila Odinga kuteuliwa bungeni kuchukua wadhifa wa kiongozi au Spika wa wengi au tukabiliane na Tsunami,” alisema.

Pendekezo la David Ole Sankok kwa bunge la kitaifa kumhusu Odinga

Kabla ya uchaguzi wa AUC uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia Jumamosi iliyopita, Ole Sankok alisema kwamba ilikuwa ni lazima kwa Odinga kushinda uchaguzi huo la sivyo angelitifua vumbi la siasa nchini baada ya kushindwa.

“Raila Odinga lazima ashinde uenyekiti wa AUC kwa sababu kushindwa kutakuwa kurusha roketi kumpandisha kwenye siasa za ndani kama Bomu la nyuklia,” alisema.

Hata hivyo, Odinga alikosa bahati ya kuibuka mshindi baada ya kujiondoa katika raundi ya 6 ya kinyang’anyiro hicho kikali.

Mgombea kutoka Djibout Mahmoud Ali Youssouf aliibuka mshindi baada ya kupata thuluthi mbili ya kura hitajika ya 33 na kumrithi mwenyekiti anayeondoka Moussa Faki.

Baada ya Odinga kubuma kwenye uchaguzi wa AUC, sasa inasubiriwa kuonekana ni mkondo upi wa kisiasa atakaochukua baada ya kurejea humu nchini wiki hii.