
MSHAURI mkuu wa masuala ya kiuchumi kwa rais William Ruto, Moses Kuria amebaini kwamba Februari 10 ilikuwa tarehe kamili na katikati baina ya siku zilizopita tangu uchaguzi mkuu na zile zilizosalia kuelekea uchaguzi mkuu.
Kupitia ukurasa wake wa X, Kuria alisema kwamba Februari 10, 2022 ni sawa na kipindi cha mapumziko kwenye mchezo wa kandanda, kwani siku ambazo zimesalia hadi kufanyika uchaguzi mkuu wa 2027 ni sawa na zile zilizopita tangu kufanyika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.
“Leo tarehe 10 Februari ni nusu saa kamili. Idadi ya siku kati ya leo na Uchaguzi Mkuu ujao ni sawa kabisa na idadi ya siku kati ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 na leo. Unachofanya na habari hii ni juu yako kabisa,” Moses Kuria alichapisha mnamo Jumatatu Februari 10.
Licha ya kutoonyesha ukakasi wowote na kauli hiyo, ilionekana na wengi kama inaelekezwa kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ambaye amegeuka kuwa mkosoaji mkuu wa uongozi wa William Ruto.
Gachagua amekuwa katika mstari wa mbele kukosoa rais Ruto na sera zake mbalimbali, tangu kung’atuliwa kwake mamlakani mnamo Oktoba mwaka jana.
Gachagua alitarajiwa kutangaza chama chake kipya wikendi iliyopita wakati wa kikao na waandishi wa habari lakini akatangaza kwamba uzinduzi wa chama chake utakuja Mei.
Kwingineko, naibu wa rais Kithure Kindiki wakati wa mkutano na wanachama kutoka kaunti ya Kiambu katika makazi rasmi ya naibu wa rais mtaani Karen alimfuma Gachagua akisema kwamba yeye ameanza siasa mapema.
Kwa mujibu wa Kindiki, Gachagua anafaa kughairi siasa hadi mwaka 2027 wakati kampeni zitazinduliwa rasmi, akimtahadharisha kwamba wakati huo ndio atajua kwamba ‘kuna wanaume hii town’.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!