Mwanamume atiwa mbaroni na polisi Homa Bay kwa tuhuma za kumuua mwanawe kwa kumnywesha petroli

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 38 katika kaunti ya Homa Bay ametiwa mbaroni na maafisa wa polisi akishukiwa kumuua bintiye mwenye umri wa miaka 7 kwa kumlazimisha kunywa petroli.


Kwa mujibu wa Ripoti za polisi, mwanamume huyo alitenda unyama huo wa kutisha Jumatatu jioni nyumbani kwake katika Kaunti Ndogo ya Ndhiwa.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans


Mwili wa mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili, ulipatikana ukioza nyumbani kwao Jumanne asubuhi ukiwa na chupa tupu ya petroli kando yake.


Bado haijabainishwa ikiwa dutu ya petroli ilikuwa na sumu.


Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Ndhiwa John Losia alisema mshukiwa ambaye alitoweka alijisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Homa Bay baada ya kutekeleza uhalifu huo.


Losia alisema wenzake huko Homa Bay walimpigia simu na kumjulisha kuwa kuna mtu alijiwasilisha kwao.


"Wenzangu huko Homa Bay walinipigia simu kuniambia kuwa mwanamume mmoja alidai kwamba alimuua mtoto wake katika eneo la Kanyikela, karibu na Sukari Industry. Niliwaambia wamzuilie ili maafisa wetu waende huko kwa sababu kulikuwa na uwezekano mkubwa kuwa yeye ndiye tuliyekuwa tukimtafuta,” Losia aliambia vyombo vya habari.


Losia aliwatuma maafisa wake katika Kituo cha Polisi cha Homa Bay na kumpeleka mshukiwa katika Kituo cha Polisi cha Ndhiwa baada ya kuidhinishwa kuwa ndiye mshukiwa wa mauaji ya mtoto huyo.


"Tuligundua kuwa yeye ndiye baba wa msichana aliyekufa. Tumempeleka Kituo cha Polisi Ndhiwa kwa mahojiano zaidi. Tutampeleka mahakamani,” Losia alisema.


Loisa alisema uchunguzi wa awali unaonyesha mtuhumiwa alimlazimisha bintiye marehemu kunywa lita moja ya petroli.