MWAKILISHI wadi wa Kileleshwa, Robert Alai ametoa maoni yake kuhusu baadhi ya watu maarufu wanaopendekezwa na kupigiwa chapuo na Wakenya kuwania urais 2027.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Alai aliwasuta wale wanaopendekeza jaji mkuu mstaafu, David Maraga kuasi maisha ya ustaafu na kujitosa kwenye siasa za Kenya.
Kwa mujibu wa Alai, yeyote anayependekeza Maraga kuwania urais hana uelewa wowote kuhusu kampeni za kisiasa humu nchini.
Alai alidai kwamba kama kweli Maraga angekuwa mgombeaji wa hakika, basi asingengoja hadi sasa hivi bila kuonyesha dalili zozote za kupiga kampeni, akisema kwamba ashachelewa sana kwani muda mwafaka wa [Maraga] kuanza kampeni ingekuwa pindi tu baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.
“Yeyote anayependekeza David Maraga kama mgombeaji urais haelewi kampeni ya kisiasa ya Kenya. Ili Maraga afuzu hata kupata robo ya kura, alipaswa kuanza kampeni za uchaguzi wa 2027 mnamo 2022,” Alai alidai.
Kwa mujibu wa mwanablogu huyo wa zamani, ni watu wapuuzi tyu ndio wenye fikira kwamba kampeni ni jambo rahisi la kuchomoka kutoka maisha ya ustaafu na kujitosa bila mpango wowote – na pengine kufaulu.
Kwa kinywa kipana, Alai alihitimisha akisema kwamba licha ya kumheshimu Maraga, lakini kibarua cha kuwania urais hakimudu hata kidogo na kuwataka watu waache kumdanganya.
“Wajinga wanafikiri kuwa kampeni za urais ni baadhi ya shughuli za kustaafu za uvivu kwa akina Methusela wa umma. Bwana Maraga hawezi kusimamia kampeni za kisiasa. Ni mkondo mwinuko wa kujifunza kwake,” alisema.
Mwaka wa 2025 umeanza kwa kasi ya juu katika ulingo wa kisiasa, baadhi ya wanasiasa akiwemo rais mwenyewe wakionekana kuvalia mawanda rasmi ya kuuza sera zao kuelekea uchaguzi wa 2027.
Makundi kadhaa yamejitokeza na kujikusanya wakiwa na lengo la kumshinda Ruto katika uchaguzi huo ambapo atalenga kutetea kiti chake kwa awamu ya pili.
Baadhi ya wakenya ambao wametangaza rasmi – na wale waliopendekezwa kuwania urais ni kama wanaharakati Okiya Omtatah na Morara Kebaso, wanasiasa Kalonzo Musyoka, Fred Matiang’i, Eugene Wamalwa bila kumsahau jaji mkuu mstaafu David Maraga.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!