RAIS William Ruto sasa anasema kwa kumfanya kuwa kiongozi wa Kenya, Mungu alimpa jukumu la kubadilisha nchi.


Akizungumza baada ya ibada katika kanisa la United Pentecostal Church of Kenya huko Dagoretti Kaskazini, Nairobi, Ruto alisema ana kila nia ya kutimiza kazi aliyopewa na Mungu.


Aliendelea kusema kuwa hiyo ndiyo sababu ya kuamua kuwafikia viongozi wote, wakiwemo wale wa upinzani, ili washirikiane katika kufanikisha mpango wa Mungu kwa nchi.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Rais alisisitiza kuwa mtu mmoja, chama cha siasa, au eneo hawezi kubadilisha nchi peke yake.


“Kuna kazi ambayo Mungu amenipa kuongoza taifa hili na jukumu la kubadilisha Kenya, na nina kila nia ya kuhakikisha tunabadilisha taifa letu. Ndiyo sababu niko tayari kufanya kazi na viongozi wote na kuwaunganisha Wakenya wote kutimiza mpango wa Mungu. Mtu mmoja, chama kimoja, eneo moja hatuwezi kufanya hivyo lakini sote tuliungana, tunaweza kuafiki mengi pamoja,” Ruto alisema.


Aliongeza kuwa yeye ni Rais wa kujivunia sana wa Jamhuri ya Kenya na anamshukuru sana Mungu kwa kuliwezesha taifa kuwa na yeye kama rais.


Ruto alizidi kuwakashifu wakosoaji ambao wamekuwa wakisema kuwa atakuwa rais wa muhula mmoja na wale wanaosema anafaa kutawala kwa zaidi ya mihula miwili.


Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Nchi, miaka michache iliyopita, wapo waliokuwa wakiamini hatawahi kuwa rais, nafasi aliyonayo sasa na anamshukuru Mungu.


“Kuna watu wanaongea mambo ya muhula mmoja, awamu mbili, awamu tatu. Pale nyuma kuna watu walifikiria sitakuwa hata na term. Nimefurahi sana Mungu amenipatia nafasi hii niwe kiongozi wa Kenya. Mimi ni Rais wa kujivunia sana wa Jamhuri ya Kenya.”


Rais aliandamana na umati wa viongozi akiwemo Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.


Wabunge kadhaa wa jiji George Aladwa(Makadara), Felix 'Jalang'o' Odiwuor(Lang'ata), John Kiarie(Dagoret Kusini), TJ Kajwang(Ruaraka), Beatrice Elachi(Dagoreti Kaskazini), Samuel Atandi(Alego Usonga), na MCAs pia walikuwepo.