Waziri wa Hazina John Mbadi, mnamo Jumamosi, alimtetea kiongozi wa chama cha ODM kuhusu matamshi yake ya awali kuhusiana na shirika la Adani Group lenye utata.

 Katikati ya Oktoba, waziri mkuu huyo wa zamani alisema kuwa shirika hilo la India lina sifa nzuri na uwezo uliothibitishwa katika miradi.

 “Adani ni mshirika anayeaminika. Wamethibitisha uwezo wao katika miradi inayopita yale tuliyoona katika Afrika Mashariki," Raila alisema huku akiunga mkono uamuzi wa awali wa serikali wa kutoa kandarasi zenye faida kubwa kwa Adani.

 Wakati akimtetea, Mbadi alibainisha kuwa mgombeaji huyo wa uenyekiti wa AUC alitambua kazi ya ajabu ya Adani Group katika baadhi ya miradi yao katika nchi nyingine.

 Alibainisha kwamba inaweza isiwe rahisi kwa mtu kuthibitisha jinsi Adani alipata mikataba katika maeneo mengine ikiwa hawaishi huko. 

“Nafikiri alichosema Raila ni kwamba Adani amefanya baadhi ya miradi katika baadhi ya maeneo ambayo yanaweza kuonekana. Kama huko Mumbai, wamefanya uwanja wa ndege bora.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

 Ikiwa walitoa hongo kwa hiyo, hatuwezi kujua. Kwani sisi tunaishi India nijue kama amehonga watu huku ile ajenge airport,” Mbadi alisema.

 Mbadi alizungumza Jumamosi katika eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu.

 Waziri alikariri kuwa Kenya bado ilikuwa katika harakati za kufanya uangalizi kabla ya kutia saini kandarasi yoyote na shirika hilo la India.

Hata hivyo, alibainisha kuwa hatua ya Marekani kumfungulia mashtaka mwanzilishi wa Adani Group Guatam Adani na washirika wengine kufuatia uchunguzi imebadili msimamo wa nchi kuhusu kuwapa kandarasi za nishati na uwanja wa ndege.

 "Ikiwa serikali ya Marekani imegundua kulikuwa na hongo, hatua bora kwa serikali yoyote inayowajibika ni kusitisha shughuli nyingine zozote na chombo kama hicho.

 

Mbadi alidokeza kuwa Kundi la Adani huenda lilificha baadhi ya taarifa kutoka kwa Kenya wakati wa mazungumzo kuhusu miradi hiyo.

 

Tulikuwa tukipitia mchakato wa uthibitishaji na uchunguzi unaostahili, na ikiwa mtu hatafichua baadhi ya nyenzo na ukweli kujihusu, ungejuaje kuwa amewahonga watu mahali pengine? Huwezi kusema,” alisema.

 

Haya yanajiri baada ya Rais William Ruto kutangaza kufutilia mbali mikataba ya JKIA na KETRACO na kampuni ya Adani Group siku ya Alhamisi.

 

Akizungumza Bungeni wakati wa Hotuba yake kwa Taifa, rais alisema uamuzi huo ulitokana na taarifa mpya zilizotolewa na vyombo vya uchunguzi na mataifa washirika.