MWANAHARAKATI Morara Kebaso amekuwa mtu wa hivi punde kutangaza rasmi azma yake kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao, 2027.

Kupitia ukurasa wake wa X, Kebaso aliandika sentensi mbili tu za kuwahakikishia wafuasi wake utayarifu wake katika kinyang’anyiro cha kuingia katika ikulu ya Nairobi.

Kiongozi huyo wa chama kipya kabisa humu nchini cha INJECT alisema kwamba ana Imani ataibuka mshindi dhidi ya washindani wake, akiwemo rais Ruto.

Kebaso alisema yeye atasimama akiwa na Imani kuu katika kabila lake ambalo alilitaja kuwa ni vijana wa kizazi cha Gen Z.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Nitawania urais wa Kenya. Kabila langu litakuwa ni vijana wa Kenya,” Kebaso alitangaza.

Tangazo lake lilijiri saa chache baada ya uvumi kuibuliwa na gazeti moja la humu nchini kuhusu aliyekuwa waziri wa masuala ya ndani Dkt Fred Matinag’i kulenga wadhifa wa urais pia.

Kebaso alionekana kutofautiana na Matinag’i akimtuhumu kuwa aliyekuwa bosi wake, rais mstaaafu Uhuru Kenyatta alihusika katika ufisadi, hivyo pia yeye [Matinag’i] hafai kuaminiwa na uongozi wa nchi.

“Bosi na mfadhili wa Matiang’I, Uhuru Kenyatta alirithi deni la trilioni 1.89 kutoka kwa Kibaki. Katika miaka kumi alikopa hadi trilioni 8.9. 80% ya pesa hizo ziliibiwa,” Kebaso alisema.

Akionyesha matumaini ya kuwa rais wa 6 wa Kenya, Kebaso alisema kwamba jambo la kwanza atakalolifanya ni kurudisha pesa za Kenya zilizoibwa na wanasiasa na kufichwa nje ya nchi.

“Mojawapo ya hatua zangu za kwanza kama Amiri Jeshi Mkuu itakuwa kurudisha pesa hizo kutoka popote pale Pandora, Visiwa vya Cayman, Jiji la Jersey, London, Hong Kong na hata hapa Kenya. Na simdanganyi na sifichi azma yangu. Ruto ni fisadi tutamjia. Lakini pia tutatafuta bilioni 12 ambazo ziliibiwa kutoka kwa hazina siku ya uchaguzi mnamo 2022,” alisema.

Alisema kwamba kuwafuata watu anaohisi ni wafisadi hakutamsaza Matiang’i – jamaa anayedaiwa kuwa mshindani mwenzake, akisema kuwa gavana wa Nyamira ni mradi wake.

“Pia tutaenda kwa mradi wa Matiang’i, Amos Nyaribo gavana wa Kaunti ya Nyamira. Chapisha tweet hii. Nikiweka biblia chini ichapishe kwenye gazeti,’ Kebaso alisema.

Wengine ambao tayari wameonyesha nia ya kuwania urais ni pamoja na Kalonzo Musyoka wa Wiper, na Eugene Wamalwa wa DAP-K.