
Kisa cha mwanamke aliyeripotiwa kutoweka kwa njia
tatanishi kiligeuka na kuwa kama filamu ya kuchekesha baada ya mwanamke huyo
kupatikana salama salimini nyumbani kwa mumewe.
Mwanamke huyo aliripotiwa kupotea na mpenzi wake
ambaye alipiga ripoti polisi kuhusu kutoweka kwake.
Baada ya msako dhidi yake kuanzishwa, alipatikana
akiwa ametulia kwa mumewe, jambo ambalo limekuwa mjadala pevu katika mitandao
ya kijamii.
Ilivyobainika, mrembo huyo aliandaa kutekwa nyara
kwake mwenyewe kwa usaidizi wa mumewe kwa nia ya kumuibia mpenzi wake pesa.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ilitoa taarifa
kamili jioni ya Jumamosi, Novemba 16, ikisimulia jinsi mshukiwa alipanga njama
na mumewe kughushi utekaji nyara.
Mpenzi mwingine wa mwanamke huyo aliwasilisha ripoti
akidai watekaji nyara walidai fidia ya Ksh150,000.
Kesi hiyo tangu wakati huo imekuwa ikivutia watu kote
nchini huku Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) na Idara ya Ujasusi (CRIB)
ikianzisha operesheni ya kumpata mwathiriwa nyara.
Uchunguzi zaidi ulipelekea wapelelezi hadi Narok
Kusini, ambapo walimpata mwathiriwa katika nyumba ya mumewe. Wawili hao tangu
wakati huo wametiwa mbaroni na polisi.
"Mnamo
Novemba 16, 2024, timu hiyo ilielekea Oldonyo Orok, Narok Kusini ambako nambari
ya mwathiriwa ilipatikana mwishowe, na kumpata nyumbani kwa mumewe,"
taarifa ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi ilisoma.
Wawili hao tangu wakati huo wamesindikizwa hadi
Nairobi, ambapo wanaweza kukabiliwa na mashtaka mazito yanayohusiana na kutoa
taarifa za uongo kwa vyombo vya sheria, kosa chini ya Kifungu cha 129 cha
Kanuni ya Adhabu.
Mapema mwezi wa Novemba, hadithi ya kutoweka kwa
mwanamke huyo ilienea mitandaoni baada ya mumewe kwenda kwenye runinga kutoa
maelezo ya kuhuzunisha lakini ya kutia shaka jinsi mkewe alishawishiwa na simu
moja.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!