
Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya amedai kuwa
mswada wa fedha wa mwaka 2024 uliotupiliwa mbali na rais Ruto mnamo Julai
umerejeshwa kisiri.
Akifichua haya kupitia ukurasa wake wa Facebook,
Salasya alisema kwamba mswada huo licha ya kutupiliwa mbali, kuna njama ya
kurudishwa na safari hii unaungwa mkono na ODM.
Salasya alisema wabunge wengi kutoka ukanda wa Mlima
Kenya wameupinga lakini akatilia mashaka kwamba chama cha ODM ndicho kinaunga
mkono kurejeshwa kwa mswada huo, akidai wameweka ahadi ya kutorekebisha hata
kikomo.
“Mswada
wa fedha wa 2024 uliotupiliwa mbali umerudi na nina furaha baadhi ya wanachama
wa serikali ya Kenya Kwanza kutoka Mt Kenya wamekataa. Adui pekee wa Wakenya ni
ODM wakiongozwa na kiongozi wao wa wengi anayesema kwamba hakuna koma inafaa
kubadilishwa kwenye mswada wa fedha wa 2024,”
Salasya alitoa kauli hiyo yenye ukakasi mwingi.
Adha, mbunge huyo alisisitiza kwamba Wakenya hawako
tayari kwa mswada huo na wanasimama kidete kuonyesha hasira zao dhidi ya mswada
huo uliotajwa kama kandamizi.
“Utakubali tena huu upuuzi mara hii ama? Tutakataa
hata kabla haujarudi kwa siri ndani ya nyumba,” mbunge huyo alisema.
Itakumbukwa mswada wa fedha wa 2024 ulitupiliwa mbali
na rais Ruto mnamo Julai baada ya msururu wa maandamano ya kuupinga ambayo
yalidumu kwa wiki kadhaa.
Maandamano hayo ambayo yalianza mnamo Juni yalifikia
kilele chake Juni 25 wakati kundi la mamia ya vijana walipovunja ua na kuingia
katika majengo ya bunge kwa fujo mno.
Machafuko hayo yalishuhudiwa kwa siku kadhaa baadae,
kupelekea rais Ruto kutupilia mbali mswada huo lakini pia kulivunja baraza lake
la mawaziri.
Baadae aliteua baraza jipya ambalo lilijumuisha
wanachama wa ODM, akiwemo John Mbadi ambaye alipewa wizara muhimu ya fedha.
Wiki iliyopita katika mahojiano kwenye runinga moja
nchini, waziri Mbadi alisema kuwa upo mpango wa kutowasilisha mswada wa fedha
wa 2025 bungeni mwaka ujao.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!