
Watahiniwa 4 wa mitihani ya kitaifa ya KCSE inayoendelea kote nchini katika shule ya wavulana ya Shiners jijini Nakuru wametiwa mbaroni baada ya kushukiwa kuhusika katika mauaji ya mtahiniwa mwenzao.
Kwa mujibu wa ripoti, mtanihiwa marehemu alifariki dunia baada ya kudungwa kisu tumboni, katika tukio hilo lililojiri shuleni humo usiku wa Jumamosi iliyopita.
Tukio hilo limewaacha wazazi na washikadau wa elimu wakiwa na maswali mengi kuhusu ni vipi mtahiniwa aliweza kuingia shuleni humo na kisu bila kugunduliwa.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo alieleza kwamba mfarakano ulizuka katika bweni lao ambapo wanafunzi hao walikuwa wanajaribu kusuluhisha baada ya bidhaa za matumizi ya mmoja wao kuibiwa.
“Wanafunzi walikuwa wanajipanga kuingia katika masomo ya ziada ya usiku, kisha tukasikia kelele hapo ndipo tulifika kwenye eneo hilo na tukapata mtahiniwa mmoja amedungwa kisu tumboni. Tulimkimbiza mvulana huyo hospitalini lakini kwa bahati mbaya alifariki njiani,” alisema mwaliku mkuu John Mwangi.
Ripoti zinasema kwamba wanafunzi wanne hao walikuwa wamefukuzwa awali, walipigana na wenzao kuhusu madai ya kuibiwa baadhi ya vitu vyao ndani ya bweni wakati walikuwa wamefukuzwa shuleni.
“Jambo kuu la hawa kupigana ni hiyo sanduku. Kuna wale wanasema sanduku ilikuwa imevunjwa, na vitu vikachukuliwa. Hivyo hao walikuwa wanataka walipwe ama waanze kulipa kisasi. Hapo ndio vita ilianzia,” mwalimu mkuu aliongeza.
Makachero wamewazuilia wanafunzi hao wanne huku uchunguzi ukianzishwa akiwemo yule aliyemdunga kisu marehemu na kutoroka shuleni.
Mtihani wa KCSE ulianza mapema wiki iliyopita na unatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba katika shule zote za upili kote nchini.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!