
Zaidi ya familia 100 katika kaunti ndogo ya Samia kaunti ya Busia wanalilia ongenezo la kunguni katika maboma yao, wakidai kwamba uvamizi wa kunguni katika malazi yao unawanyma usingizi kwa muda sasa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kutia huruma iliyopeperushwa kwenye runinga ya KBC, wakaazi hao ambao ni waathirika walifichua kwamba kero la uvamizi wa kunguni limekuwa kizungumkuti kwao kwa zaidi ya miaka 2 sasa.
Wanawake hao walikuwa wanatoa kero zao wakati wa mchakato wa kufukizia kunguni hao ambao uliongozwa na kundi la wanawake wa Busia, Samia Women Achievers, shughuli iliyopewa mada ‘Angamiza Kunguni’.
Naibu kamishna wa Funyula, Joyce Onguso aliongoza shughuli hiyo na kutoa wito kwa wahisani wengine kutoka duniani kueneza misaada yao kwa waathirika wa kunguni katika kaunti ya Busia.
“Tumenaza huku leo tukiendelea mbele, kuna maboma mengi sana yameathirika kwa kuvamiwa na kunguni, na pia chawa. Tutatembea katika maboma mengi sana ambayo tumesikia yako na shida na kufanya yale ambayo tunaweza kama kina mama wa Busia,” alisema DCC Onguso.
“Nimejaribu kubadili malazi lakini bado kunguni hawaishi, mpaka kwa nyumba ndani kwa ukuta wako tu, ninaomba kama mnaweza tusaidia,” alisema Gerald Khalande, mkaazi wa Samia.
“Tatizo la kunguni ni janga ambalo liko hapa Samia, ambalo linataka nguvu na sisi peke yetu kama CBO hatuwezi, tunataka msaada kutoka kila mahali, mwneye anaweza kutusaidia, wahisani njooni tusaidiane,” aliongeza Merlin Achieng kutoka kundi la Samia Women Achievers.
Kero la kunguni si tatizo tu ambalo linashuhudiwa katika eneo hilo la Magharibi bali ni tatizo ambalo limezua usumbufu kwa mamia ya watu hata katika mataifa yaliyoendelea.
Itakumbukwa, mwezi Oktoba mwaka 2022, vyombo mbalimbali vya habari kote duniani viliripoti kuhusu kero la kunguni katika jiji kuu la Ufaransa, Paris.
Uvamizi huo ulianza kabla ya Wiki ya Mitindo ya Paris, wakati ripoti zilipoibuka za kuongezeka kwa kuonekana kwa wadudu hao majumbani, kwenye sinema, kwenye treni na hata hospitalini. Jiji hilo si geni kwa wasafiri—Paris ndilo jiji linalotembelewa zaidi duniani na watalii milioni 44 mwaka wa 2022.
Wala si geni kwa kunguni: kati ya 2017 na 2022, zaidi ya kaya moja kati ya 10 za Ufaransa ziliripoti kushambuliwa na kunguni, kulingana na ANSES, wakala wa afya na usalama wa Ufaransa.
Lakini ANSES inaripoti kwamba "kuongezeka kwa mashambulizi ya kunguni katika miaka ya hivi karibuni kumetokana hasa na kuongezeka kwa usafiri na kuongezeka kwa upinzani wa kunguni kwa dawa".
Kwa maneno mengine, kunguni hawa wamebadilika na kuwa kunguni wakubwa: wamebadilika ili kuunda ulinzi na urekebishaji dhidi ya kemikali fulani zinazotumiwa kuwaangamiza.
Wadudu hao kwa kawaida hukaa kwenye magodoro na fremu za kitanda, wakiwavizia wanadamu kulala kabla ya kutambaa na kunyonya damu kwa ajili ya chai yao.
Lakini pia wanaweza kusafiri kupitia wanadamu, wakipanda mavazi, masanduku na mizigo ya mkononi ili kusafiri ulimwengu na kuchunguza upeo mpya.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!