Waziri wa fedha John Mbadi anasema serikali itakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kubatilisha uuzaji wa hisa zake za asilimia 15 katika kampuni ya Safaricom PLC. Akizungumza na vyombo vya habari mjini Kisumu mapema leo, Mbadi alisema serikali itapinga uamuzi huo uliotangaza kuwa shughuli hiyo yenye thamani ya mabilioni ya pesa ilikiuka katiba. Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu liliamua jana kuwa mchakato huo wa kuuza hisa haukukidhi matakwa ya kisheria na ya kikatiba, ikiwemo ushirikishwaji wa maana wa umma.