Wakenya wanatarajiwa kulipa zaidi kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kama nepi za watoto, mafuta ya kupikia, simu za mkononi na mitungi ya gesi baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuruhusu Kenya kuendelea kutoza ushuru wa juu kwa bidhaa hizo kwa mwaka mwingine.

Hatua hiyo ilianza kutekelezwa Julai Mosi na inalenga kulinda viwanda vya ndani pamoja na kuongeza mapato ya serikali.

Bidhaa zingine zitakazoathirika ni gesi, mafuta ya kulainisha mitambo, nyaya za optic fibre, bidhaa za chuma na magari.

…………………..

Kenya imepanua ushirikiano wake wa biashara ya umeme na Ethiopia baada ya Kenya Power kutia saini mkataba mpya wa ununuzi wa umeme na Ethiopian Electric Utility (EEU).

Mkataba huo uliotiwa saini mjini Addis Ababa unaweka mfumo mpya wa kibiashara wa kusafirisha umeme kutoka Ethiopia kuja hapa nchini kupitia njia ya usafirishaji wa umeme ya HVDC ya kilovolti 500, mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya usambazaji wa umeme barani Afrika.

Chini ya makubaliano hayo, Kenya itanunua umeme kwa gharama ya karibu shilingi 19.50 kwa kila kilowati, huku mkataba huo ukitarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa bei nafuu na wa uhakika nchini.