Zaidi ya muongo mmoja baada ya Kenya kupandishwa hadhi na kuwa nchi ya uchumi wa mapato ya kati, taifa bado limeshindwa kufikia kiwango kinachofuata cha maendeleo ya kiuchumi.

Ripoti ya hivi punde ya Benki ya Dunia imeendelea kuiweka Kenya katika kundi hilo, licha ya mataifa sita kupandishwa hadhi.

Kwa sasa, mapato ya taifa kwa kila mtu nchini Kenya yanakadiriwa kuwa dola 2,200, kiwango ambacho bado kiko chini ya kiwango kinachohitajika kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa mapato ya juu ya kati.

………………

Mataifa ya Kenya na Umoja wa Ulaya yamezindua mpango wa kuongeza mara mbili thamani ya biashara na uwekezaji kati yao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Hatua hiyo inajengwa juu ya mafanikio ya Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Kenya na Umoja wa Ulaya ulioanza kutekelezwa Julai 2024 na ambao umechangia ongezeko la asilimia 20 la biashara.

Mkakati huo wa utekelezaji wa miaka 10 unalenga kuwasaidia wafanyabiashara, wazalishaji, wakulima na wawekezaji wa Kenya kunufaika kikamilifu na fursa ya kuuza bidhaa bila ushuru wala vizuizi vya kiwango katika soko la nchi 27 za Umoja wa Ulaya.

Katibu Mkuu wa Biashara, Regina Ombam, amesema mpango huo ni hatua muhimu ya kuhakikisha mkataba huo unaleta manufaa halisi ya kiuchumi kwa Kenya.