NAIROBI, KENYA, Julai 28, 2025 — Rais William Ruto amesema kuwa serikali yake imejitolea kuhakikisha kuwa elimu ya msingi na sekondari inapatikana kwa kila mtoto bila vizingiti vyovyote, akisema kuwa ni haki na si hisani.

Kauli hii inakuja baada ya Waziri wa Hazina, John Mbadi, kuashiria kwamba mzigo wa kugharamia elimu ni mzito mno kwa serikali.

Ruto alisema kuwa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ni haki ya kila mtoto, na kwamba serikali yake imewekeza katika miundombinu, walimu na ufadhili.

Katika hotuba yake alipohudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la ACK St. Martin’s Light Industries, Kariobangi, Ruto aliahidi kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha mpango wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo.

Akitaja elimu kuwa “zawadi kuu kabisa jamii inaweza kumpa kijana,” Rais alisema kuwa mpango huo hautasalimishwa wala kupunguzwa.

“Elimu ya msingi bila malipo ni haki ya kila Mkenya. Tumechukua hatua nyingi katika miaka miwili iliyopita kuhakikisha kuwa elimu hii inapatikana kwa wote,” alisema Rais Ruto alipohudhuria ibada katika Kanisa la ACK St Martin’s Light Industries, Kariobangi.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Alieleza kuwa serikali imewekeza pakubwa katika ujenzi wa madarasa mapya hasa mijini ili kukabiliana na msongamano, na kuongeza kuwa zaidi ya walimu 70,000 wameajiriwa tangu 2022.

“Hatutaacha mwanafunzi yeyote nyuma. Tunapanga kuwaajiri walimu wengine 24,000 mwaka ujao,” aliongeza.

Kuhusu utulivu katika sekta ya elimu, Rais alirejelea makubaliano ya mkataba wa pamoja (CBA) na walimu hadi mwaka 2029, ambayo yanalenga kuzuia migomo ya mara kwa mara.

“Nawahakikishia kuwa upatikanaji na ubora wa elimu haviwezi kuvurugwa,” alisema Ruto, akiweka wazi kuwa serikali yake inalenga kuhakikisha elimu inakuwa bora, jumuishi na yenye manufaa kwa maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, Waziri wa Hazina John Mbadi alizua mjadala mkali wiki iliyopita alipowaarifu wabunge kuwa hali ya kifedha ya serikali haitaruhusu kugharamia kikamilifu mpango wa elimu bila malipo.

“Mzigo wa kuendesha elimu bila malipo ni mkubwa mno kwa serikali. Hali hii huenda ikawalazimu wazazi kuchangia zaidi,” alisema Mbadi mbele ya Kamati ya Bunge.