LARI, KIAMBU, Julai 23, 2025Mazishi ya mchekeshaji maarufu wa mtandaoni, KK Mwenyewe, yaligeuka kuwa ya mtafaruku na sintofahamu baada ya waombolezaji kumzomea Dennis Itumbi, Mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Uchumi wa Ubunifu, kwa madai ya kutoa ahadi zisizotekelezwa kwa wabunifu wa maudhui nchini.

Maziko hayo yaliyofanyika katika kijiji cha asili cha mchekeshaji huyo huko Lari, Kaunti ya Kiambu, yalihudhuriwa na maelfu ya watu wakiwemo familia, mashabiki, na wanamaudhui kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mazingira ya huzuni na ukungu wa asubuhi vilitawala hafla hiyo, ambapo wengi walifika kuaga kijana aliyejulikana kwa ucheshi wa kumwigiza aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kupitia video fupi-fupi za mtandaoni.

Dennis Itumbi nyumbani kwa KK Mwenyewe

Itumbi: Maudhui Yake Yanaendelea Kuishi

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Akizungumza mbele ya umati uliogubikwa na majonzi, Itumbi alimsifu KK Mwenyewe kama miongoni mwa wanamaudhui waliobadilisha tasnia ya burudani kwa njia ya kipekee.

“Baada ya kifo cha KK, kinachotufariji ni kuwa maudhui yake bado yatatufurahisha na kutuunganisha,” alisema Itumbi.

“Niko hapa kumuaga kijana aliyetuunganisha kwa kicheko.”

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kujitahidi kuboresha mazingira ya kazi kwa wabunifu:

“Changamoto kubwa ni jinsi wabunifu watafaidika kifedha na kazi zao. Tangu serikali ya sasa iingie madarakani, tayari tumeanza mazungumzo na mitandao kama Facebook ili walipe wabunifu wa Kenya.”

Neno la “Wantam” Lamtikisa

Hata hivyo, hali ilibadilika mara moja baada ya Itumbi kutaja ahadi za malipo kwa wabunifu. Mmoja wa waombolezaji alipaza sauti kwa nguvu akisema: “Wantam!”, kauli maarufu ya kukashifu maneno ya viongozi yanayoonekana kuwa hewa.

Ndani ya dakika chache, kelele na vigelegele vya kejeli vilienea huku waombolezaji wengine wakisema kwa hasira:

Wakiendelea kumzomea, baadhi walimwambia aache kutumia majukwaa ya maombolezi kutoa ahadi mpya ambazo hawana imani nazo.

Akitetea msimamo wake, Itumbi alisema:

“Siamini kama kelele hizi zinatoka kwa wabunifu wa kweli. Uundaji wa maudhui ni kazi ya maisha.”

Kauli hiyo haikufua dafu, kwani ilizidi kuchochea ghadhabu ya waliokuwepo, na ndiposa mazingira yakawa ya taharuki kiasi cha kusimamisha hotuba hiyo kwa muda.

Mama ya KK Mwenyewe

Ahadi Mpya Zatolewa

Katika juhudi za kutuliza hali, Itumbi alieleza kuwa serikali imetengeneza mfumo mpya wa kusaidia wabunifu ambao hawajafaidika kifedha na maudhui yao:

“Kwa wale ambao akaunti zao hazijaanza kulipwa na Facebook, tumeanzisha jukwaa maalum la President Creatives ili kushughulikia changamoto hizo,” alisema.

Pia alitangaza mpango wa kuanzisha chama cha kuweka na kukopa kwa wabunifu:

“Mchekeshaji maarufu Kabugi ataongoza mpango wa kuanzisha Sacco ya wabunifu ambayo itarahisisha usaidizi wa serikali kwa vipaji vya kidijitali,” aliongeza.

Mshereheshaji Aingilia

Kufuatia hali hiyo, mshereheshaji wa hafla alilazimika kuingilia kati akiwataka waombolezaji kutoa nafasi ya usikilizaji kwa kila mmoja:

“Naomba tafadhali, tafadhali tusikilizane. Si pia tumepea hawa wengine nafasi waongee,” aliomba kwa unyenyekevu.

Licha ya jitihada hizo, ukimya haukurejea kikamilifu huku minong’ono na misemo ya dhihaka ikiendelea kusikika hadi hafla hiyo ilipofikia tamati.

KK Mwenyewe

Mjadala Waibuka

Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu namna serikali inavyoshughulikia maslahi ya wanamaudhui nchini.

Wengi wanahoji kuhusu utekelezaji wa sera mbalimbali zinazolenga kuwafaidi wabunifu wa kidijitali, hasa wakati ambapo umaarufu wao hauna uwiano na mafanikio ya kifedha.

Kwa mara nyingine tena, sauti ya “Wantam!” imegeuka kuwa si neno la mzaha tu, bali ishara ya kutoridhika kwa kizazi cha kidijitali chenye matarajio makubwa kwa serikali.