NAIROBI, KENYA, Julai 23, 2025 — Mkewe aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Bi Dorcas Rigathi, amejitokeza hadharani kupinga vikali madai yanayoenea mitandaoni na katika duru za kisiasa kwamba yeye ndiye anayemwongoza na kumshinikiza mumewe katika maamuzi ya kisiasa.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyofanyika Kanisa la Christ the Foundation Ministries mjini Nairobi, Bi Dorcas alitaja madai hayo kama ya kipuuzi, ya kubuniwa na yenye lengo la kumdhalilisha mumewe, ambaye kwa sasa ni kiongozi mkuu wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP).

“Sijawahi kumkalia mume wangu, sijawahi kumwongoza katika maamuzi yake. Rigathi ni kiongozi kamili, mwenye msimamo na maono yake binafsi,” alisema Dorcas kwa msisitizo, akiongeza kuwa wana ndoa yao kwa misingi ya usawa, heshima na maombi.

Bi Dorcas, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihusika katika shughuli za kijamii na kiroho, alisema kuwa wanawake wana nafasi muhimu katika jamii, lakini hilo halimaanishi kwamba wanawavunjia heshima waume zao.

“Kwa kuwa ninamuunga mkono mume wangu hadharani na kumsindikiza kwenye shughuli zake za kijamii au kisiasa, haimaanishi kwamba namwelekeza au ninamtawala. Hiyo ni dhana potovu,” aliongeza.

Dorcas Gachagua

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Madai yachochea mijadala mitandaoni

Madai hayo yameibuka wakati ambapo Rigathi Gachagua anaendeleza ziara yake ya kisiasa nchini Marekani, huku akizidi kujiimarisha kama sauti ya upinzani dhidi ya Rais William Ruto.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakimkejeli Gachagua kwa madai kuwa hana msimamo wa kisiasa na kwamba anaendeshwa kisiri na mkewe — dhana ambayo Bi Dorcas amesema imejengwa na watu wasiopenda kuona familia thabiti ikiongoza.

“Wanawake wakisimama na waume zao kwa uthabiti, jamii huanza kuwa na mashaka. Lakini mimi sitatikiswa na maneno ya ovyo. Nitazidi kumuombea mume wangu na taifa letu,” alisema huku akipokelewa kwa makofi na waumini waliokuwepo.

Wandani wake wamtetea

Baadhi ya viongozi wa DCP wametetea Bi Dorcas, wakisema kuwa anapotoshwa kwa makusudi na wapinzani wa kisiasa. Walimtaja kuwa mfano bora wa wake wa viongozi wanaojitokeza kusaidia jamii bila kutaka madaraka ya kisiasa.

Taarifa hiyo imekuja huku Wakenya wakisubiri kwa hamu kurejea kwa Gachagua kutoka Marekani, ambapo anatarajiwa kueleza msimamo wake kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa taifa.