Mwanawe Rais William Ruto, George Ruto, ameirejesha matatu yake maarufu inayojulikana kama Mood gerejini kwa ajili ya matengenezo, baada ya baadhi ya sehemu zake kuripotiwa kuharibika wakati wa uzinduzi wake rasmi katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) mwishoni mwa juma.
Matatu hiyo, iliyovutia umati mkubwa kutokana na muundo wake wa kuvutia na vipengele vya kisasa kama vile paneli za jua, inasemekana ilipata uharibifu kutokana na msisimko uliopitiliza wa baadhi ya walioudhuria hafla hiyo.
Hali hiyo ilithibitishwa kupitia chapisho kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa moja ya akaunti zinazohusiana na Mood, ambapo video fupi ilichapishwa Jumatatu ikionyesha gari hilo likiwa gerezani likifanyiwa matengenezo.

“Mood kwa sasa iko nje kwa marekebisho madogo. Tutarejea hivi karibuni,” ilisomeka maelezo yaliyoandamana na video hiyo, na kuzua maswali kutoka kwa mashabiki waliotaka kujua kwa nini matatu hiyo tayari ilikuwa inahitaji matengenezo.
Mtumiaji mmoja aliuliza, “Kuliendaje? Mbona tayari iko gerejini?” Akaunti hiyo ilijibu kwa kueleza kuwa uharibifu ulitokana na vurugu na shangwe zilizoshuhudiwa wakati wa uzinduzi huo.
Wahudumu wa Mood waliongeza kuwa haikuwa matatu hiyo pekee iliyopata uharibifu.
“Matatu nyingi ziliharibika kwa kiwango fulani, nazo pia zinapitia marekebisho. Ilitokana na msisimko… ungeliona paneli za jua?” ilisomeka sehemu ya jibu lao.
Miongoni mwa uharibifu uliozungumziwa sana ni ule wa paneli za jua zilizowekwa kwenye Mood, ambazo zilitangazwa sana kabla ya uzinduzi huo.
Vipengele vingine vilivyovutia mno kuhusu matatu hiyo ni skrini ya runinga ya inchi 65, dawati la DJ kwa muziki wa moja kwa moja, paneli za jua, na viti vya kifahari aina ya bucket seats vilivyoagizwa kutoka China.
Hii ndiyo matatu ya kwanza nchini Kenya kuwa na viti vya bucket katika mpangilio wa viti 25, hatua inayopunguza idadi ya kawaida ya viti 32 ili kutoa nafasi zaidi na starehe kwa abiria.

Mpangilio huo wa viti ni wa mfumo wa 2-kwa-1, ukiambatana na jukwaa la DJ ndani ya matatu kwa lengo la kuboresha hali ya usafiri au burudani wakati wa hafla.
Wakati huo huo, mamia ya vijana walihudhuria hafla hiyo katika KICC kuonyesha uungwaji mkono wao kwa mwana wa Rais na kusherehekea utamaduni wa matatu.
Baada ya tamasha kukamilika, eneo la katikati ya jiji (CBD) liligubikwa na msongamano wakati matatu hiyo ilipochukua doria fupi jijini.
Mamia ya vijana waliandamana na matatu hiyo, na kusababisha msongamano mkubwa wa magari katika maeneo ya karibu uliodumu kwa saa kadhaa hadi usiku wa manane.
Vurugu hizo zilisababisha taharuki kwa wakazi wa Nairobi waliokuwa wakielekea nyumbani, huku baadhi ya ripoti zikiwataka wakaazi kuwa makini na magenge ya kihuni.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!