Mwanaume ameripotiwa kupigwa risasi na kuuawa katika eneo la Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Inadaiwa kuwa mwanaume huyo alipigwa risasi mbili, moja shingoni na nyingine kifuanu, wakati wa maandamano yanayoendelea ya Saba Saba.

Anaripotiwa kufariki kutokana na majeraha ya risasi baada ya kukimbizwa katika hospitali ya umma iliyo ndani ya mji wa Kitengela.

“Mwanaume huyo alipigwa risasi shingoni na kifuani walipokuwa kwenye makabiliano ya kurushiana mawe na polisi kando ya Barabara ya Prison. Alitangazwa kufariki dunia katika hospitali alikokuwa amekimbizwa,” chanzo kiliiambia Radio Jambo.

Mwanaume mwingine anaripotiwa kujeruhiwa kwa risasi mguuni wakati wa maandamano hayo.

Inasemekana alikimbizwa katika hospitali hiyo hiyo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Awali, maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia waliokuwa wamejihami waliingilia kati baada ya vijana wa kizazi cha Gen Z kuingia mitaani takriban saa nne asubuhi siku ya Jumatatu.

Vijana hao waliokuwa wakiandamana walifunga Barabara ya Nairobi–Namanga na kusababisha kusimama kwa usafiri katika barabara hiyo kuu ambayo ilikuwa na shughuli za kawaida asubuhi ya mapema.

Waliwasha moto kwa kutumia matairi kabla ya polisi kufika eneo hilo. Polisi wanatumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Maduka yote yameendelea kufungwa huku polisi wakiendelea kukabiliana na waandamanaji. Kikosi cha GSU kimeimarisha nguvu kwa kuungana na wenzao kukabiliana na waandamanaji hao.

Magari mawili ya polisi ya maji ya kuzima ghasia pia yamepelekwa kushughulikia hali hiyo mjini Kitengela.

Mapema asubuhi hii, maafisa zaidi wa polisi walipelekwa mjini Kitengela huku vizuizi vya barabarani vikiwekwa katika maeneo maalum kando ya Barabara ya Namanga.

Hali ni tofauti katika mji jirani wa Athi River ulioko Kaunti ya Machakos ambako hali ni ya kawaida. Mji wa Athi River umeendelea kuwa tulivu huku shughuli za kibiashara zikiendelea kama kawaida.