Mbunge wa Belgut Nelson Koech amedai kuwa kusitishwa kwa muda kwa huduma ya treni ya abiria ya Madaraka Express ya saa 4 usiku kutoka Mombasa hadi Nairobi siku ya Jumapili kulitokana na tishio la shambulio.

Koech alisema taarifa za kijasusi zilionyesha kuwepo kwa mpango wa kushambulia abiria waliokuwa wakisafiri kwa treni hiyo ya usiku kwenye reli ya kisasa ya SGR.

“Kulikuwa na taarifa za kijasusi kwamba kulikuwa na kundi la watu waliotaka kushambulia treni hiyo na vijana waliokuwemo ndani na kisha kulilaumu serikali,” alidai kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga cha humu nchini.

Shirika la Reli la Kenya liliomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa lakini halikutoa maelezo ya haraka kuhusu aina ya hitilafu ya kiufundi au ni lini huduma hiyo itarejelewa.

“Tunasikitika kuwajulisha wananchi kuwa kutokana na changamoto za kiufundi, huduma ya treni ya abiria ya Madaraka Express ya saa 4 usiku kutoka Mombasa hadi Nairobi imesitishwa,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Abiria walioathirika walishauriwa kufika kituo cha Mombasa kufikia saa 2 asubuhi ya Jumatatu kwa ajili ya kusafiri.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kusitishwa kwa ghafla kwa huduma hiyo kulitokea baada ya maafisa wa polisi kuweka vizuizi barabarani kwenye barabara ya Mombasa-Diani wakilenga vijana waliokuwa wakirejea kutoka tamasha la Diani Summer Tide, jambo lililosababisha msongamano mkubwa wa magari.

Inaripotiwa kuwa mamlaka zilichukua hatua hiyo kufuatia taarifa za kijasusi zilizodokeza kuwa baadhi ya vijana waliokuwa ndani ya magari hayo—ambao wengi wao walisikika wakipaza sauti “Wantam”—walikuwa na mpango wa kusafiri hadi Nairobi kushiriki maadhimisho ya Saba Saba siku ya Jumatatu.

Vizuizi hivyo vya barabarani vilikuwa bado vimeimarishwa jijini Nairobi na viunga vyake kufikia asubuhi ya Jumatatu, hali iliyowalazimu baadhi ya raia kutembea umbali mrefu kufika kazini.