Naibu Inspekta Jenerali (DIG) Gilbert Masengeli amepuuzilia mbali madai kuwa Wakenya wanazuiwa kuingia katika eneo la Biashara Kuu la Jiji la Nairobi (CBD), akisema kuwa hakuna vizuizi vyovyote kwa watu kuingia jijini.
Uchunguzi wetu ulidhihirisha kuwa kufikia saa 12:30 asubuhi, barabara kuu kadhaa jijini Nairobi zilikuwa zimefungwa huku polisi wakiongeza juhudi za kuzuia watu kuingia maeneo nyeti.
Barabara zilizoripotiwa kufungwa ni pamoja na Thika Road maeneo ya Roysambu na Guru Nanak, Wayaki Way katika daraja la Kangemi, Mombasa Road karibu na GM Motors, Ngong Road katika mzunguko wa City Mortuary, Valley Road karibu na Wizara ya Ulinzi na Integrity Centre, Juja Road katika Pangani Interchange, na Lang’ata Road karibu na T-Mall.
Usalama pia umeimarishwa katika makutano ya barabara kuu.
Uwepo mkubwa wa polisi ulionekana katika mzunguko wa barabara ya Uhuru Highway na Kenyatta Avenue, Uhuru Highway na Haile Selassie, Moi Avenue, Kenyatta Avenue, na karibu na Barabara ya Bunge na Harambee Avenue.
Doria za polisi pia zilionekana katikati ya jiji, ikiwemo Barabara ya Ronald Ngala na River Road.
Maeneo yaliyozuiwa karibu na Bunge, City Hall, na Ikulu yaliendelea kufungwa chini ya ulinzi mkali.
Ripoti zilionesha kuwa idadi ya watu jijini ilikuwa ndogo, ingawa mamlaka zinatarajia ongezeko kadri siku inavyoendelea.
Polisi wamewashauri wananchi kuepuka eneo la biashara katikati ya jiji na kutumia njia mbadala.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!