Mwanablogu aliyekuwa ametoweka, Ndiangui Kinyangia, amefikishwa katika mahakama ya Milimani, jijini Nairobi.
Mama yake aliangua kilio alipomkumbatia mwanawe ambaye amekuwa akitafutwa kwa zaidi ya wiki moja sasa. Ndiangui aliingia mahakamani akiandamana na mawakili Kibe Mungai na wakili wa ngazi ya juu Martha Karua.

Jaji Chacha Mwita alikuwa ameagiza Jumanne kwamba blogger huyo afikishwe mahakamani akiwa hai au akiwa amekufa.
Wakili wa familia Wahome Thuku alisema mapema Alhamisi kwamba Ndiangui aliwasiliana na familia Jumanne jioni, akieleza kuwa yuko salama.
"Kwa niaba ya familia ya Bw. Ndiangui Kinyagia, ningependa kuarifu umma wa Wakenya kwamba Bw. Ndiangui ambaye alipotea wiki iliyopita ameweza kuwasiliana na familia na kwamba yuko salama, mwenye afya njema na hali yake ni nzuri. Bw. Ndiangui alimpigia simu mmoja wa jamaa zake Jumanne jioni kutoka eneo lisilojulikana," ilisoma taarifa hiyo.

Wahome alisema kuwa Ndiangui alieleza jamaa huyo wa familia kuwa alijificha kwa muda kwa hofu ya maisha yake baada ya kupata taarifa kuwa maafisa wa DCI walikuwa wakimtafuta kuhusiana na tuhuma za jinai ambazo hazijabainishwa.
"Bw. Ndiangui ameonyesha kuwa yuko tayari na anataka kujisalimisha kwa DCI na kufikishwa mbele ya mahakama yoyote iwapo usalama wake utahakikishwa.
"Tumemshauri afike katika Mahakama Kuu ya Milimani leo, Alhamisi tarehe 3 Julai 2025 saa tano asubuhi," alisema.

Thuku alisema kuwa taarifa hiyo imewasilishwa rasmi kwa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) kwa uchambuzi na kuwasilishwa mahakamani.
"Tunataka kuwakumbusha umma kuwa DCI walivunja mlango wa nyumba yake wakati hakuwepo na kuchukua baadhi ya vitu, na kwamba familia iliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kinoo.
"Familia ya Bw. Ndiangui inawashukuru Wakenya wote walioko ndani na nje ya nchi kwa usaidizi wao katika kipindi hiki kigumu. Ni matumaini yetu na maombi yetu kuwa haki itatendeka katika suala hili," alisema.

Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!