Msemaji wa Serikali, Isaac Mwaura, amefichua kuwa serikali imeweka mikakati mahususi ya kuzuia waliokwepa kulipa Hustler Fund wasijiandikishe kwa mpango wa bima ya afya ya SHA.
Katika mahojiano na kituo moja cha radio humu nchini, Mwaura alisisitiza kuwa takribani shilingi bilioni 6 ambazo hazijalipwa kutoka kwa mikopo ya Hustler Fund ni kiwango kikubwa cha fedha ambacho serikali inakusudia kukusanya ili kufadhili maendeleo.
Kando na kuhakikisha urejeshwaji wa mikopo hiyo, alieleza kuwa mkakati huo pia utaanzisha uhusiano wa kifedha kati ya Hustler Fund na michango ya SHA.
“Hustler Fund ni nzuri, inawawezesha wananchi kulipia ada zao za SHA kwa mwaka mzima na hiyo inatufaa zaidi,” alisema Isaac Mwaura.
Mwaura pia alieleza mikakati ya serikali ya kuhakikisha uandikishaji na utekelezaji mzuri wa mpango wa SHA, huku akihamasisha watu wenye kipato cha chini kukumbatia mpango wa Lipa SHA Pole Pole, ambao hukusanya zaidi ya shilingi milioni 30 kila siku, kama njia ya kuwawezesha kulipia kidogo kidogo bila kulemewa kifedha.
“Kuna wale ambao hawana kazi za malipo ya kila mwezi. Lipa SHA Pole Pole ni njia kwao kulipa bila mashinikizo ya kifedha,” alisema Msemaji huyo.
Kwa mujibu wa Mwaura, SHA huandikisha zaidi ya watu 50,000 kila siku, na michango yao imeiwezesha serikali kulipa zaidi ya shilingi bilioni 18 kutoka kwa deni la NHIF la shilingi bilioni 33.
Mwaura alisisitiza tena dhamira ya serikali ya kufanikisha huduma ya afya kwa wote kupitia SHA, ambayo aliielezea kuwa mpango wa bima ya afya unaofanya vizuri zaidi nchini Kenya.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!