Nuru Okanga, MCA mtarajiwa wa Kholera Ward, Kakamega//FACEBOOK

MCA mtarajiwa wa wadi ya Kholera, Nuru Okanga amedai kwamba atakuwa MCA wa kwanza humu nchini kuwasilisha mswada wa kutaka kupunguzwa kwa mishahara ya MCAs.

Okanga, ambaye amekuwa akiweka matumaini yake hai ya kuchaguliwa kama MCA katika kaunti ya Kakamega katika uchaguzi mkuu ujao wa 2027, alisema kwamba MCAs hawafai kuwa na mishahara mikubwa kwani kazi nyingi kwenye kaunti hufanywa na magavana.

Alisema kuwa ikiwa atachaguliwa, wiki ya kwanza ofisini itakuwa ya kutayarisha mswada wa kupunguzwa kwa mishahara ya wawakilishi wadi, huku akiwasuta kwa kutaka nyongeza zaidi.

“Juzi nimeona MCAs wakisema eti wanataka waongezewe mishahara, ya kazi gani? kununua magari makubwa makubwa? Kwanza nataka mimi nikiwa MCA, nikichaguliwa hivi pap, napeleka mswada kwa bunge, mshahara wa MCA upunguzwe,” Okanga alifoka.

“Urudi chini! Kwa sababu MCA ni kazi gani anafanya? Kazi nyingi kaunti ndio inafanya kutoka kwa kulima barabara, hadi vitu vingine. Hivyo MCAs wanafaa watuambie, kwanza mimi nikichaguliwa nitapeleka miswada kali kali kwa bunge,” aliongeza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Akihojiwa iwapo hatua hiyo haitamsababishia chuki kutoka kwa viongozi wenzake, Okanga alisema kwamba masilahi yake yatakuwa kwa wananchi na si kwa viongozi wenzake.

‘Mimi nitakuwa n a masilahi ya watu wangu, wewe kiongozi nichukie lakini kwa ground niko sawa. Mimi nafuata ground, sifuati kiongozi. Na ground ndio imeniweka hapo. Watu wamefeli kwa sababu wamefuata viongozi. Mimi nikichaguliwa nitakaa na watu wa chini,” alisema huku akitolea mfano wa jinsi mbunge Peter Salasya anatangamana na wananchi.

Kauli yake kuhusu kupunguzwa kwa mishahara ya MCAs inakuja wiki chache baada ya MCAs katika kongamano lao Nairobi kudai nyongeza ya hadi 700% ya mishahara.

Wakizungumza katika siku ya mwisho ya Mkutano wa 5 wa Bunge la Kaunti jijini Nairobi, wabunge hao pia waliazimia kushinikiza kutekelezwa kwa Hazina ya Maendeleo ya Wadi na uhuru wa kifedha kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kaunti, wakisema kuwa hatua hizi ni muhimu kwa uangalizi mzuri na utoaji wa huduma.