Kalonzo Musyoka na Raila Odinga//FACEBOOK

KIONGOZI wa upinzani Kalonzo Musyoka amesisitiza kwamba urafiki wake na kinara wa ODM, Raila Odinga bado uko pale pale licha ya Odinga kujiondoa upinzani na kuafikiana kufanya kazi pamoja na rais Ruto serikalini.

Akizungumza Nairobi siku moja iliyopita, Kalonzo alisema kwamba muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ulikufa rasmi wakati ODM ilipotia saini ya ubia na UDA.

Kulingana na Kalonzo, Azimio haiwezi endelea kuwepo wakati vyama tanzu vimejiondoa na kuacha vyama vichache ndani yake, WIPER kikiwa miongoni mwa vichache vilivyobaki.

“Ambacho kilikuwa Azimio la Umoja One Kenya – na huu ni ukweli mchungu – marafiki wetu katika ODM walitia saini na UDA nje ya KICC, kwa maoni yangu ile ilithibitisha mwisho wa Azimio,” Kalonzo alisema.

“Ni lazima tuwe wakweli kwa sababu WIPER haiwezi kusalia katika Azimio peke yake. Hivyo hii ni taarifa ya kweli,’ aliongeza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Musyoka hata hivyo alibainisha kwamba licha ya Odinga ‘kusaliti’ upinzani na kutimukia serikalini, hakuna siku mtu yeyote atamsikia akimdhihaki na kumzomea kwa kile alikitaja kuwa huo sio utaratibu wake.

“Hata hivyo, tunaishi katika hili taifa, tumejenga mahusiano ya Kibinafsi na heshima kwa kila mmoja. Hakuna mtu atawahi nilisikia nikimshambulia Raila Odinga kwa sababu hiyo sio DNA yangu,” alisema.

Kiongozi huyo alisisitiza umuhimu wa kuheshimu misimamo ya kila mmoja.

Kalonzo amesalia kuwa moja kati ya sauti chache za upinzani zinazokosoa serikali baada yam wanachama mkuu wa Azimio, ODM kuanza kucheza densi ya serikali.

Upinzani kwa sasa umebaki mikononi mwa Wiper ya Kalonzo Musyoka, DAP-K ya Eugene Wamalwa, PLP ya Marth Karua, Jubilee inayoongozwa na katibu mkuu Jeremiah Kioni, INJECT ya Morara Kebaso na aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua ambaye anatarajiwa kuzindua chama chake kipya mwezi Mei.

Japo ODM wamekuwa wakisisitiza kuwa upinzani, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakiradidi Kauli kwamba chama hicho kimo ndani ya serikali kwani baadhi ya wanachama wake wamekabidhiwa nyadhifa mbalimbali chini ya serikali ya rais William Ruto.