Methu na Ichung'wah watupiana vijembe Facebook//FB

SAA chache baada ya baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya kufokewa katika ziara ya kimaendeleo ya rais Ruto katika eneo hilo, lawama zilianza kurushwa, kila mmoja akionekana kumlaumu mwenzake kwa dhihaka hiyo mbele ya rais.

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa, Kimani Ichung’wah ambaye alifokewa katika kaunti ya Nyandaru alitupiana vijembe na seneta wa kaunti hiyo.

Kupitia mitandao wa Facebook, Seneta John Methu alichapisha ujumbe wa kebehi akimpa pole mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah kwa kufokewa na watu kiasi kwamba alilazimika kukatisha hotuba yake mbele ya rais Ruto.

Methu alitilia msumari moto kwenye donda bichi la Ichung’wah kwa kumwambia kwamba Nyandarua hawapendi masuala ya kitoto.

“Kimani Ichung’wah pole sana kaka, Nyandaru hatupendi utoto,” Seneta Methu aliandika.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Ichung’wah naye hakukaa kinyonge, alimlenga Methu kwa mshale huku akionekana kukejeli nywele zake.

Ichung’wah japo alimshukuru Methu kwa pole zake, alimkumbusha kwamba wakati mwingine atakaporudi katika kaunti ya Nyandarua, atajihami na mashine ya kunyoa nywele.

“Ahsante sana, nitarudi tu na kinyozi,” Ichung’wah alimjibu.

Methu na Ichung'wah watupiana vijembe Facebook//Screenshot-Facebook

Awali, Methu aliibua madai kwamba viongozi hao walifokewa lakini rais hakufokewa kwa vile ni yeye tu aliyekuwa amelipia hadhira.

Rais Ruto ameingia katika siku yake ya nne ya ziara ya kimaendeleo katika eneo hilo ambalo limempa mapokezi makubwa licha ya awali kudhaniwa kwamba hangepokelewa vizuri kutokana na uhasama wake wa kisiasa na aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua.

Mapokezi yake na halaiki hata hivyo yalifafanuliwa na gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ambaye alisema watu walijitokeza kwa wingi kwa sababu ya marupurupu na zawadi na wala si ishara ya kutikisa ngome ya Gachagua.