
UNHCR, Shirika la umoja wa kimataifa linaloshughulikia masilahi ya wakimbizi na wato wasiokuwa na makazi ya kudumu limeungana na mashirika mengine ya kutetea haki za kibinadamu kutoa wito kwa sekta za kibinafsi kuwajumuisha watu hao katika mipango ya kiuchumi.
Wito huu ulitolewa katika mkutano ulioleta pamoja viongozi wa biashara lililoandaliwa kwa pamoja na UNHCR na Muungano wa Amahoro, kujadili jukumu la sekta ya kibinafsi katika kushughulikia suala la uhamishaji wa kulazimishwa.
Kikao hicho kilianzisha Kongamano lijalo la Sekta ya Kibinafsi ya Afrika kuhusu Uhamisho wa Kulazimishwa, linalopangwa kufanyika Aprili 29, 2025, jijini Nairobi.
UNHCR na shirika la Amahoro walionyesha wasiwasi wao jinsi wakimbizi wanavyobaguliwa katika uwezeshaji wa kiuchumi katika mataifa mbalimbali barani Afrika.
Katika miaka ya hivi karibuni, bara la Afrika limeshuhudia ongezeko la watu wasiokuwa na makazi ya kudumu, takwimu hizo zikikadiriwa kuwa watu milioni 45.
Mashirika hayo yalitoa ombi la sekta binafsi kuwajumuisha wakimbizi katika mipango ya kupata mikopo ya kuanzisha biashara na hata ufikiaji wa kazi kwa michakato iliyorahisishwa.
"Kongamano hili ni sehemu ya vuguvugu linalokua katika bara zima," alisema Nancy Aburi, Mkuu wa Ushirikiano wa Sekta ya Kibinafsi Afrika, UNHCR.
"Wafanyabiashara wanatambua kuwa ujumuishi sio tu kuhusu uwajibikaji - ni faida ya kimkakati. Wakati makampuni yanapoingia 'all in,' yanasaidia kuunda masoko yenye nguvu na imara zaidi."

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa shirika la Amahoro, Isaac Kwoku alisisitiza kuwa makundi ya Afrika yalizokimbia makazi yana uwezo mkubwa wa kiuchumi.
"Kuunganisha wakimbizi katika minyororo ya ugavi na mikakati ya biashara sio hisani - ni biashara nzuri. Kampuni zinazokubali hili hupata maarifa mapya, kupanua masoko, na kukuza ukuaji wa sekta," alisema.
Katika kongamano hilo, makampuni mengine kama benki ya Equity na kampuni ya mawasiliano yaliwakilishwa.
Saralyn Wairumi, Mkurugenzi Mshiriki katika Benki ya Equity Ltd, aliangazia usaidizi wa muongo mzima wa benki kwa uhamishaji fedha, benki katika eneo la wakimbizi, na fedha jumuishi. "Tumethibitisha kuwa huduma za kifedha zinaweza kubadilisha maisha na jamii," alisema.
Karen Basiye, Mkurugenzi wa Biashara Endelevu na Maendeleo ya Kijamii katika Safaricom PLC, aliunga mkono maoni hayo.
"Mabadiliko ya kweli hutokea wakati wafanyabiashara wanaona wakimbizi kama washirika, na sio walengwa tu. Wako tayari kuchangia, kujenga biashara, na kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi," alisema.
UNHCR ilianzishwa mwaka 1950 na inaongoza juhudi za kimataifa kuhakikisha watu waliokimbia makazi yao wanapata ulinzi, makazi, na upatikanaji wa elimu na huduma za afya, na fursa ya kujenga upya maisha yao. Kufanya kazi katika nchi zaidi ya 130.
Kwa upande wao, shirika la Amahoro lilianzishwa mwaka wa 2019 na limekuwa muunganishi mkuu wa viongozi wa sekta binafsi wa Afrika kwa athari chanya za kijamii.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!